‘Uvuvi haramu una athari kwa walaji samaki’
DAR ES SALAAM; WAVUVI nchini wametakiwa kufuata kanuni za uvuvi na kuachana na uvuvi haramu kwani una athari kubwa kwa walaji wa samaki.
Kauli hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi Kikosi cha Wanamaji Tanzania, Moshi Sokoro, akizungumza na HabariLEO na kuongeza kuwa uvuvi haramu wa kutumia nyavu ndogo ‘kokoro’ ndiyo unaongoza katika matukio ya uhalifu wa uvuvi haramu.
Amesema licha ya kokoro makosa mengine wanayokutana nayo ni utumiaji wa baruti wakati wa kuvua samaki.
Amesema katika kudhibiti hali hiyo kwa kipindi cha 2022 na 2023, watuhumiwa 17 wamekamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
“Baadhi ya makosa yametolewa uamuzi na watuhumiwa kulipa faini mahakamani, mengine majalada yapo chini ya upelelezi,” amesema.
“Sasa tukifanya uvuvi haramu maana yake tunaua mazalia ya samaki kama makokoro na baruti kwa kuwa yanaenda kuvunja matumbawe na miamba ambayo inajijenga kwa muda mrefu na ndipo yaliopo mazalia ya samaki. Unapoivunja maana yake hata mayai ya samaki au samaki wanakosa sehemu ya kutagia.
“Kwa hiyo mwisho wa siku tutakuwa na bahari ambayo haina samaki,” amesema.