Uwanja wa ndege wa Iringa na safari mpya angani

Safari za anga za ndege kubwa katika Kiwanja cha Ndege cha Iringa zinatarajiwa kurejea tena rasmi Februari 22 mwaka huu, baada ya kusitishwa kwa zaidi ya miaka nane ili kupisha upanuzi na ukarabati wa miundombinu.

Hatua hii inatarajiwa kuboresha huduma za usafiri wa anga mkoani Iringa, kurahisisha safari za abiria na kuinua uchumi wa eneo hilo kupitia biashara na utalii.

Safari hizo zitaanza na ndege za Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) Bombadier Dash -8 Q400 na kufuatiwa na ndege za Precision Air zinazotarajia kuanza safari zake Machi 3, mwaka huu.

Advertisement

Kwa mujibu wa Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Iringa, Ashraph Mohamed, ndege za ATCL zitafanya safari kati ya Dar es Salaam – Iringa – Dar es Salaam mara tatu kwa wiki na Precision Air nazo zikifanya safari zake kati ya Dar es Dalaam Dodoma na Iringa mara tatu pia kwa wiki.

Akizungumza mara ya kutembelea kiwanja hicho, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, alisema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha sekta ya usafiri wa anga mkoani humo, ikilenga kuboresha huduma kwa wakazi wa Iringa na mikoa jirani.

Alisema mradi wa upanuzi wa kiwanja hicho ni mojawapo ya viwanja 16 vilivyoainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka 15, uliozinduliwa mwaka 2011.

Alisema uboreshaji wa kiwanja hicho umefanyika kupitia programu ya pili ya uboreshaji wa sekta ya usafirishaji, ambayo inalenga kuchochea maendeleo kupitia sekta za utalii, kilimo, na madini.

“Ninawahimiza wakazi wa Iringa kutumia usafiri huu wa anga kwa wingi ili kuhakikisha kuwa huduma hizi zinadumu na hatimaye kuongezeka kutoka siku tatu kwa wiki hadi safari za kila siku,” alisema Waziri Mbarawa.

Alisema usafiri wa anga ni njia salama na ya haraka ya kusafiri, hasa kwa safari za dharura kama vile huduma za afya.

“Kurudi kwa huduma za ATCL na ujio wa mashirika mengine kama Precision Air na Auric Air kutatoa chaguo zaidi kwa wasafiri na kupunguza gharama za usafiri wa anga kwa wananchi wa Iringa na maeneo ya jirani,” alisema.

Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Iringa alifafanua kuwa kiwanja hicho sasa kina uwezo wa kufanya kazi mchana na usiku baada ya kufungwa kwa mifumo ya taa za kuongozea ndege kwenye njia za kutua na kuruka ndege.

Aidha alisema ukarabati huo ulihusisha pia ujenzi wa barabara ya kutua na kurukia yenye urefu wa mita 2,100 na upana wa mita 30, barabara ya maungio, maegesho ya ndege, mifumo na mitambo ya kuongoza ndege, kituo cha zimamoto, jengo la abiria, kituo cha umeme, uzio na maboresho mengi.

Alisema kiwanja hicho kwasasa kina uwezo wa kuhudumia ndege kubwa mbili za Bombardier pamoja na ndege ndogo tano aina ya Caravan kwa wakati mmoja.

Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Iringa Peter Serukamba katika ukaguzi wa kiwanja hicho, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dk Linda Salekwa alisema mafanikio ya uboreshaji wa Uwanja wa Ndege wa Iringa yanafungua milango kwa fursa nyingi.

Alizitaja fursa hizo kuwa ni pamoja na kuimarika kwa sekta ya utalii Iringa ambako ni lango kuu la Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na utalii wa kusini.

Alisema usafiri wa anga utarahisisha safari za watalii kutoka Dar es Salaam na maeneo mengine, jambo ambalo litachochea ukuaji wa sekta ya hoteli, huduma za watalii, na biashara zinazohusiana na utalii.

Aidha alisema kurudi kwa safari za ndege kutawezesha wafanyabiashara kusafirisha bidhaa kwa haraka, kuvutia wawekezaji wapya, na kuimarisha shughuli za kiuchumi mkoani Iringa.

“Biashara za kilimo, madini, na viwanda vidogo zitapata manufaa makubwa kutokana na urahisi wa usafirishaji wa bidhaa na huduma,” alisema

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *