Uwekezaji afya uenziwe, uwe endelevu

JUZI Rais Samia alipokea Tuzo ya Gate Goalkeeper iliyotolewa na Taasisi ya Gates Foundation Dar es Salaam kutambua mchango wake katika sekta ya afya hususani mapambano dhidi ya vifo vya wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano.

Kwa upande wake, Rais Samia Suluhu Hassan alisema tuzo hiyo ni ya Watanzania wote hasa watumishi wa sekta ya afya ambao wamekuwa wakijitoa kwa kufanya kazi kwa bidii na weledi hali iliyowezesha kupunguza idadi ya vifo vya wanaofika hospitali kujifungua.

Pamoja na kwamba ni tuzo iliyotokana na juhudi za wahudumu wa afya kuanzia madaktari, wataalamu, wauguzi, wakunga na wote wanaotoa huduma katika sekta hiyo, bado uwekezaji madhubuti uliofanywa na serikali ni chachu kubwa ya mafanikio.

Advertisement

Chini ya uongozi wa Rais Samia, serikali inastahili pongezi nyingi kutokana na kujielekeza katika kuimarisha huduma za afya kwa kuwekeza maeneo mbalimbali.

Kwa mfano, takwimu zinaonesha ambavyo serikali imejizatiti kuongeza idadi ya hospitali zenye vitengo vya dharura kutoka saba hadi 130.

Imeongeza huduma za mama na mtoto kutoka vituo 340 mwaka 2020 hadi 523 mwaka 2024, upatikanaji wa huduma za afya umetoka asilimia 73 mwaka 2020 hadi asilimia 86 mwaka 2024.

Uwekezaji huu unadhihirisha dhamira ya dhati ya serikali katika kuhakikisha kwamba kila Mtanzania, hususani wanawake na watoto, anapata huduma bora za afya.

Kupungua kwa vifo vya wajawazito na watoto ni uthibisho wa huduma za afya kuimarika nchini. Juhudi hizi za uwekezaji katika kuboresha huduma za afya ni za kupigiwa mfano.

Serikali imewekeza katika kuboresha miundombinu ya afya, kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya na kuweka sera ambazo zitasaidia katika kupunguza vifo na kuboresha maisha ya wananchi.

Tunazidi kumpongeza Rais Samia kwa kuweka bayana utayari wa serikali kuendelea kuwekeza katika afya katika kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.

Kwa msimamo huu wa Rais Samia sambamba na ufanisi wa huduma katika sekta ya afya, ni bayana kuwa matarajio ya kuongeza umri wa kuishi kufikia miaka 75, kuimarisha lishe, afya ya uzazi na kupunguza vifo vya wajawazito na watoto zaidi yatatimia.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *