UWT Geita watakiwa kuacha kinyongo uchaguzi mkuu

VIONGOZI na wanachama wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Geita wameonywa kutotumika kama chambo cha kueneza fitina kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.

Aidha wanachama wa UWT mkoani Geita wametakiwa kuunganisha nguvu na kuwaunga mkono bila ‘kinyongo’ watia nia na wagombea wanawake wenye uwezo watakaoingia kwenye kinyang’anyiro cha uongozi.

Mwenyekiti wa UWT mkoa wa Geita, Laurencia Bukwimba ametoa angalizo hilo wakati katika mkutano maalum wa wajumbe wa UWT mkoa uliofanyika mjini Geita.

“Mwanamke anapogombea nafasi basi sisi pamoja tuwe mstari wa mbele kuhakikisha kwamba mwanamke huyu anafanikiwa kwa sababu mafanikio yake ndio mafanikio yetu sisi wote”, amesema.

Bukwimba amesema kuelekea kupata viongozi wapya kuanzia kura za maoni hadi uchaguzi mkuu kuna maneno mengi ya fitina huibuka ambayo UWT wanapaswa kuyakataa ili kulinda umoja na mshikamano.

“Tunaposikia maneno tuwe na ngozi ngumu, unaposikia maneno kuwa flani kafanya hivi ama vile simamia kile ambacho unaamini kuwa hiki ni sahihi.

“Naomba sote tuwe makini, kama kuna watu ambao wanapotosha mambo, basi sisi tusimamie ukweli na kwenye haki, kwa kuzingatia kanuni na taratibu za Chama Cha Mpainduzi”, amesema Bukwimba.

Amesema mshikamano ukikosekana ndio chanzo cha mgawanyiko ndani ya chama jambo ambalo ni kinyume na linakinzana na kanuni za katiba na ilani ya CCM.

Bukwimba amewasisitiza wanawake wote mkoani humo kuwa mstari wa mbele kujitokeza kuboresha taarifa katika daftari la kudumu la mpiga kura na hata kuchukua fomu za uongozi kuwania nafasi tofauti.

“Tugombee nafasi ili tupate fursa sisi kama wanawake kuweza kushiriki kikamirifu katika uongozi wa taifa letu, na nidpo tutakapopata fursa ya kuhamasisha kutoa maamuzi mbalimbali”, amesema Bukwimba.

Diwani wa viti maalum Wilaya ya Mbogwe, Pili Meshack amekiri iwapo wanawake wataungana wana nafasi kubwa kuchukua nafasi za uongozi wa ngazi udiwani na ubunge bila hata kutegemea nafasi za viti maalum.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button