UWT Geita watakiwa kuwa mabalozi wa serikali

MBUNGE wa Viti Maalum mkoani Geita, Rose Busiga ameuomba Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) mkoani hapa kuwa mabalozi wa serikali kwa kutangaza na kuunga mkono mipango ya Rais Samia Suluhu.

Busiga amesema hayo leo wakati akizungumuza na wananchi pamoja na viongozi wa UWT Mkoa wa Geita katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Nyakafuru wilayani Mbogwe.

Advertisement

Amesema serikali ya awamu ya sita imejipambanua kufikia adhima ya kuboresha huduma kwenye sekta mbalimbali ili kumfanya mtanzania aweze kunufaika na nchi yake hivo ni vyema kina mama waisemee.

“Serikali ya awamu ya sita ipo kazini, na niwahakikishie wakazi wa Geita, hususani wanawake, ninaomba tumuunge mkono mheshimiwa Rais, yupo anafanya kazi na hawezi kutuangusha, tuwe na imani.”

Akikagua ujenzi wa ofisi ya UWT Mbogwe, Busiga ameahidi kuwaunga mkono wanawake wilayani humo kukamilisha mradi huo ili kuboresha utendaji na uwajibikaji wa UWT kufanya kazi katika mfumo rasmi.

Aidha Busiga amegawa kompyuta pamoja na mashine ya kunakili na kuchapisha taarifa kwa ofisi zote za UWT ngazi za wilaya mkoani hapa ili kuimarisha utendaji wa jumuiya hiyo iweze kujiendesha kisasa.

Mbunge wa viti maalum mkoa wa Tabora, Jackline Kainja amesema wanawake ni jeshi kubwa na iwapo wataungana na kusimama na serikali yao basi watahamasisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Ghati Chomete ameipongeza UWT mkoani Geita na kuwaomba kuendelea kuwaunga mkono wabunge wao ambao wameonyesha dhamira ya dhati katika uwajibikaji.

Katibu wa UWT wilaya ya Mbogwe, Amina Mohamed amesema bajeti ya ujenzi wa ofisi ya UWT wilayani humo ni Sh milioni 80 na hadi sasa imetumika Sh milioni 30 na ujenzi umefikia hatua ya upauaji.

1 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *