TUME Huru ya Uchaguzi Tanzania (INEC) imetangaza kusogezwa mbele kwa uzinduzi wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura uliokuwa ufanyike Julai Mosi mkoani Kigoma hivyo sasa utaanza Julai 20.
Mwenyekiti wa (INEC Jaji Jacobs Mwambegele ametangaza hatua hiyo katika mkutano na waandishi wa Habari mjini Kigoma akisema kusogezwa mbele kwa zoezi hilo kunatokana na wadau wa uchaguzi waliotaka kupewa muda zaidi kushiriki kutoa elimu na kuhamasisha jamii kujitokeza kwa wingi kushiriki uboreshaji daftari.
Jaji Mwambegele amesema kabla ya kusogezwa mbele tayari tume imefanya mikutano tisa na wadau mbalimbali kati ya hiyo minane imefanyika Dar es Salaam na mmoja mkoani Kigoma.
Amesema mipango ya uzinduzi wa uboresahji huo kufanyika mkoani Kigoma inaendelea kama ilivyopangwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa anatarajia kuwa mgeni rasmi.
Soma zaidi:https://habarileo.co.tz/wadau-wa-uchaguzi-waikingia-kifua-tamisemi/
Aidha mwenyekiti huyo wa Tume ameziomba asasi kuomba jukumu la kutoa elimu na uhamasishaji huku akiwataka viongozi wa vyama vya siasa, dini na wadau wa uchaguzi kushiriki kikamilifu kutoa elimu kwa jamii lakini pia kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi mchakato wa uboreshaji daftari la kudumu la wapiga kura utakapoanza.
Mkurugenzi wa Asasi isiyo ya kiserikali ya Green shadow ya mjini Kigoma, Ignas kilongola amesema wadau watatumia muda huo kuona namna wanavyoweza kufanikisha kusaidia mchakato huo.