VETA washauriwa kupanua ushirikiano kuongeza ujuzi

DAR ES SALAAM: Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amekitaka Chuo cha Ufundi na Mafunzo Stadi (VETA) kujenga ushirikiano na kampuni zilizopo sokoni ili kuelewa mahitaji ya soko na ujuzi unaohitajika lengo ni kuboresha sekta ya ufundi stadi ambayo imekuwa mkombozi wa ajira nchini.

Prof. Mkenda ameyasema hayo wakati akizungumza na wadau wa sekta ya nguo na mavazi katika kongamano maalum lililofanyika kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 ya VETA.

Alisisitiza kuwa ili kufanikisha azma ya kuandaa vijana wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira, ni lazima VETA iwe na mahusiano ya karibu na kampuni za uzalishaji ili kubaini mahitaji halisi ya sekta hiyo.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia anayeshughulikia Elimu, Dk. Charles Mahera amesema mkutano huo utawasaidia wadau kupanua ujuzi wao ili kuendana na mahitaji ya viwanda. Pia alibainisha kuwa hatua hiyo itaongeza thamani ya mazao kama vile pamba na ngozi.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesisitiza kuwa sekta ya ufundi stadi imeajiri Watanzania wengi. Aliongeza kuwa VETA itaendelea kutimiza wajibu wake wa kutoa ujuzi unaohitajika kwa wananchi wengi zaidi ili kusaidia upanuzi wa fursa za ajira nchini.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button