Vietnam kuwaachia huru wafungwa 8,000

HANOI: SERIKALI ya Vietnam imepanga kuwaachia huru wafungwa zaidi ya 8,000, wakiwemo raia 25 wa kigeni kutoka mataifa tisa, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanguka kwa Saigon mnamo Aprili 30, 1975.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mtandao wa Habari wa Serikali ya Vietnam, wafungwa hao wataanza kuachiwa kuanzia Alhamisi, ingawa haijafahamika nchi za asili za raia hao wa kigeni.

Naibu Mwenyekiti wa Ofisi ya Rais, Pham Thanh Ha, amesema msamaha huo ni ishara ya ukarimu wa taifa hilo na unalenga kuendeleza utamaduni wa ubinadamu na sera ya huruma ya chama tawala cha Kikomunisti pamoja na serikali ya Vietnam.

Hata hivyo, chini ya sheria za nchi hiyo, wafungwa waliopatikana na hatia ya kujaribu kuipindua serikali ya kikomunisti au makosa ya ugaidi hawajumuishwi katika mpango huo wa msamaha. SOMA : Tanzania, Vietnam kuongeza ushirikiano wa kiuchumi

Maadhimisho ya Aprili 30 mwaka huu yataadhimisha miaka 50 tangu majeshi ya Vietnam Kaskazini, yaliyoongozwa na Wakomunisti, yalipoiteka Saigon (sasa Ho Chi Minh City) na hivyo kuhitimisha vita vya Vietnam kwa ushindi dhidi ya Vietnam Kusini iliyokuwa ikiungwa mkono na Marekani.

Tukio hilo linaendelea kuwa na uzito mkubwa katika historia ya taifa hilo, likikumbukwa kama siku ya kuungana kwa nchi na mwanzo wa enzi mpya chini ya utawala wa Kikomunisti.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button