MKOA wa Mtwara umefanikiwa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kutoka 17 Julai hadi Septemba mpaka 9 Oktoba hadi Disemba 2023.
Yameelezwa hayo wakati wa kikao cha tathmini ya vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga kilichofanyika katika halmashauri ya mji wa Nanyamba mkoani humo.
Kikao hicho ni cha robo ya Oktoba hadi Desemba 2023, kilichokutanisha wataalam wa sekta hiyo kutoka halmashauri zote tisa mkoani humo.
Kufuatia hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas ameendelea kuwasisitiza wataalam wa sekta hiyo kuwa, taarifa hizo za vifo vya mama na mtoto ziwe ni ajenda ya kudumu kwenye vikao vyote vya kisheria.
“Isiwe tu inatolewa taarifa lakini itolewe taarifa ikieleza na sababu za kifo hicho kilichotokea na hatua gani zimechukukiwa” amesema Abbas
Aidha amewaagiza wakurugenzi, watendaji wa halmashauri hizo kulipia gharama za mafunzo yanayoratibiwa na mkoa huo kupitia taasisi mbalimbali zinazolenga kuboresha huduma ya uzazi salama.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Frank Omollo amesema katika robo ya kwanza Januari hadi Machi 2023 vifo hivyo vilikuwa 24 na Aprili hadi Juni katika mwaka huo ni vifo 22.
Aidha siyo tu mafanikio katika robo hizo lakini pia mwaka 2021 kulikuwa na vifo 75, 2022 84 na 2023 vifo 67, mafanikio yaliyotokana na kuwepo kwa jitihada mbalimbali za kuhakikisha vifo hivyo vinapungua kwa kiasi kikubwa ikiwemo uimarishaji wa mfumo wa usimamizi.
Hata hivyo, ufatiliaji wa uwajibikaji kwa wataalam, watoa huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya zimeongezeka, utoaji wa elimu kwa jamii kuhusu akina mama wajawazito wawahi kwenye vituo vya kutolea huduma.
pia akina mama hao inapofika hatua ya kujifungua wakajifungulie katika vituo cha afya, uimarishaji wa upatikanaji wa damu salama katika halmashauri.
“Sisi mkoa tunafatilia kwa karibu na halmashauri zetu, kwahiyo imesaidia kupunguza ule uzembe kwa sehemu kubwa”amesema Omollo
Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto mkoani humo, Ashura Ausi amesema katika ufatiliaji wa suala hilo wamekuwa na kanzidata inayojumuisha wataalam kutoka halmashauri hizo zote kwenye mkoa huo.
Lengo ni kufatilia kila mama mjamzito atayekuwa anaingia katika kituo cha afya ili kupeana taarifa endapo mama huyo atakuwa na changamoto yoyote iweze kufanyiwa kazi kwa urahisi zaidi.