MTWARA; CHAMA Kikuu cha Ushirika cha Masasi Mtwara (MAMCU) mkoani Mtwara kimewasimamisha watendaji wawili akiwemo mhasibu mkuu wa chama hicho kwa kukiuka agizo la serikali la kutaka wakulima wa korosho kulipwa malipo yao ndani ya siku saba baada ya kuuza korosho zao.
Mwenyekiti wa chama hicho Alhaji Mfaume amewaambia waandishi wa habari Jumatano wiki hii kuwa chama hicho kimefuatilia na kugundua kuwa watendaji hao wanafanya hujuma kwenye malipo ya wakulima.
“Tumefuatilia vya kutosha na kujiridhisha kuwa kuna hujuma ambayo hawa wahasibu wanafanya na tumeamua kuwaondoa kazini,” amesema.
Wiki moja kabla ya kuanza kwa minada ya korosho Oktoba 11 mwaka huu, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alifanya mkutano na Bodi ya Korosho nchini na vyama vya ushirika na wadau wengine kwenye tasnia ya korosho na kutaka vyama vikuu vya ushirika kusimamia na kulipa wakulima malipo wakati wa minada.
Alivitaka vyama hivyo kulipa malipo hayo ndani ya siku za saba za kazi mara baada ya wakulima kuuza korosho zao kwenye minada.
Mfaume amesema baada ya waziri kutoa agizo hilo, chama cha MAMCU kilichukua hatua na kuelimisha watendaji wakiwemo wahasibu ili waweze kusimamia na kutekeleza agizo la waziri kwa ufasaha.
“Kama chama kikuu cha MAMCU na kutambua unyeti wa agizo la Waziri, tulichukua hatua tukawapa watendaji wetu semina hasa wahasibu na kuwaambia kama kuna eneo tunatakiwa tuongeze utendaji ni suala la uhasibu,” amesema.