Jumla ya vijana 174 wakiwemo wanawake 26 wamehitimu mafunzo ya jeshi la akiba wilayani Ileje, mkoa wa Songwe.
Wanaume waliohitimu mafunzo hayo ni 148.
Akifunga mafunzo hayo katika kata ya Isongole, Ileje, Jumatatu, Mkuu wa wilaya hiyo, Farida Mgomi alisisitiza juu ya umuhimu wa kutumia mafunzo hayo kuleta mabadiliko chanya katika jamii ikiwemo kuibua maovu katika jamii lakini pia kutekeleza majukumu wanayopewa na viongozi wao pasina kujali hali.
Mgomi ametoa rai kwa wahitimu wote kushiriki kikamilifu katika suala zima la utunzaji wa amani hasa kipindi hiki ambacho nchi inaelekea katika zoezi la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.
Katika hatua nyingine, DC Mgomi aliwahakikishia wahitimu hao kuwa Serikali inatambua changamoto zilizopo hususan wakati wa mafunzo hivyo kupitia ofisi yake.
Alisema changamoto za wahitimu zimepokelewa kama zilivyoainishwa katika risala iliyosomwa mbele yake na kuahidi kuzifanyia kazi huku akisisitza kuendelea kutambua nafasi ya Jeshi la Akiba katika jamii na Taifa kwa ujumla.