Vijana 350 wapata ajira kampuni ya parachichi

NJOMBE: VIJANA 350 wa Kitanzania wameajiriwa kwenye kampuni ya parachichi ya AVO AFRICA iliyopo mjini Makambako mkoani Njombe.
Kampuni hiyo inayojishughulisha na ununuzi na usafirishaji wa parachichi, imesaidia kutatua changamoto ya ajira kwa vijana hao na kupunguza idadi ya wasio na ajira.

Hayo yameelezwa na Ofisa Rasilimali Watu na Utawala wa kampuni hiyo, Omega Kabuje, wakati akizungumza na Maofisa Habari, Mawasiliano, Uhusiano na Itifaki serikalini waliopo mkoani Njombe kwa ajili ya kikao kazi, walipofanya ziara ya kujifunza kuhusu uzalishaji na uchakataji wa zao la parachichi.
Amesema kampuni hiyo imejikita katika ununuzi wa zao la parachichi kutoka kwa wakulima wakubwa na wadogo kutoka maeneo mbalimbali ya mikoa ya Njombe, Iringa, Mbeya, Arusha, Kilimanjaro na Kagera, jambo ambalo limewanufaisha wakulima wengi wa maeneo hayo.

“Hadi sasa tumeweza kuwafikia wakulima zaidi ya 4,000 na kukusanya matunda kwa asilimia 60 kutoka kwa wakulima,” amesema Kabuje.

Kabuje amesema Kampuni ya AVO AFRICA baada ya kununua parachichi kutoka kwa wakulima, husafirisha matunda hayo mabichi kwenda mataifa mbalimbali duniani ikiwemo nchi za Ulaya, Singapore, India, Saudi Arabia pamoja na Dubai.



