VIJANA 420 kutoka mikao 13 nchini wamefundishwa kudhibiti sumu kuvu kwa kutengeneza vihenge vya chuma ili kumsaidia mkulima anapovuna na kukausha mazao yake ayahifadhi kwenye sehemu salama.
Mratibu wa Mradi wa sumu kuvu kutoka Mamlaka ya Elimu ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Joseph Kimako amesema hayo alipozungumza na HabariLEO katika maonesho ya Nanenane kitaifa yanayoendelea mkoani Mbeya.
Kimako amesema katika mradi huo mamlaka hiyo inashughulika na kipengele cha baada ya kuvuna katika sehemu ya kuhifadhi.
Amesema vijana hao watakapomaliza mafunzo yao watapewa vifaa vya bure ili waweze kujiajiri kwa kutengeneza vihenge hivyo.
“Lakini mkulima atakuwa amesaidiwa kwa sababu vijana watakuwa na nyenzo za kuweza kutengeneza vihenge kule kwenye mazingira yao,” amesema.
Amesema mradi huo VETA imeingia makubaliano na Wizara ya Kilimo, katika eneo hilo la kuzuia athari ya sumukuvu kwenye mazao ya nafaka.
Naye Meneja Uhusiano wa mamlaka hiyo, Sitta Peter alisema wamekuwa wakitengeneza program mbalimbali zinazolenga makundi mbalimbali ya kwenye jamii na kwenye kilimo.
“Kwenye mradi huu lengo ni kufanya uhifadhi wa mazao uwe ni bora kwa kutumia hivyo vihenge vya chuma, hivyo kudhibiti sumukuvu ambayo ina athiri mazao ya aina mbalimbali ikiwemo mahindi karanga na mazao mengine ya nafaka,” amesema.