Vijana Dodoma wachangamkia fursa za mikopo

Vijana wakijadiliana namna ya kuinua biashara zao.

KWA Mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, idadi ya vijana nchini ni asilimia 34.5 ya Watanzania wote na kati yao, asilimia 21.7 wanafanya kazi zisizo na ujuzi.

Kutokana na hali hiyo, serikali imefanya juhudi kubwa kuwekeza kwa vijana kwa kuwasaidia kupata fursa zinazojitokeza zikiwamo za kiuchumi na ajira.

Hizi ni pamoja na kuwapa mikopo ya asilimia nne kutoka halmashauri na mikopo yenye masharti nafuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.

Advertisement

Licha ya jitihada hizo, vijana wengi hawana uelewa kuhusu fursa hizo na namna ya kuzitumia. Ili kuhakikisha vijana wanatumia vema fursa zilizo mbele yao, Taasisi ya Mulika Tanzania imeanzisha mpango wa kuwawezesha kiuchumi katika wilaya nne za Mkoa wa Dodoma kupitia mafunzo maalumu yanayolenga kukuza ujuzi wa biashara, usimamizi wa fedha na upatikanaji wa fursa za kiuchumi.

Mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) kuwezesha vijana kiuchumi kupitia ujasiriamali na upatikanaji wa fursa za ajira, hivyo kusaidia kutokomeza umasikini. Hata hivyo licha ya juhudi hizo, vijana wanakutana na changamoto kadhaa katika kupata huduma za afya ikiwa ni pamoja na haki za afya ya uzazi na jinsia (SRHR), elimu na fursa za kiuchumi.

Akizungumza wakati wa mafunzo maalumu kwa vijana wa Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, Ofisa Biashara wa Wilaya hiyo, Grace Nkalalwe anasema wilaya hiyo ina fursa nyingi za biashara zinazoweza kunufaisha vijana na kuwakomboa kiuchumi.

“Katika wilaya yetu ya Chamwino kuna fursa nyingi za kibiashara ikiwemo kilimo cha zabibu na pia halmashauri inatoa mikopo kwa vijana,” anasema. Anasema kijana anapaswa kuangalia fursa zilizopo katika maeneo yanayomzunguka ili kuanzisha biashara hata kama ni ndogo.

Ofisa Biashara Wilaya ya Chamwino jijini Dodoma, Grace Nkalalwe akizungumza na vijana kuhusu namna ya kupata fursa za biashara.

“Kabla ya kuanzisha biashara yoyote unapaswa kuangalia soko, …kufanya hivyo kutakusaidia kupata faida kwenye biashara yako,” anasema Nkalalwe. Akifafanua kuhusu fursa za mikopo, Ofisa Mikopo wa wilaya hiyo, Mary Muhoza anasema serikali ilitoa tamko la kuhakikisha inawezesha wananchi wake kiuchumi ili kupunguza umasikini.

Anasema kila halmashauri ilielekezwa kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani inayotolewa mara nne kila mwaka kwa ajili ya mikopo kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu. Muhoza anasema katika mikopo hiyo asilimia nne ni za wanawake, asilimia nne za vijana na mbili kwa wenye ulemavu.

“Kwa vijana ili upate mkopo ni lazima muunde kikundi cha watu watano, muwe na wazo la biashara, muwe pia na katiba ya kikundi, pia muweze kusajili kikundi kwenye mfumo na mwisho ni kuomba mkopo kupitia huo huo mfumo,” anafafanua Muhoza.

Ofisa Maendeleo Kata ya Buigiri, wilayani Chamwino, Veronica Baluwa anatoa angalizo kwa vijana kuhakikisha wanakuwa na mradi wa pamoja kabla ya kuomba mkopo. “Angalizo kwa wanakikundi; mnatakiwa kuwa na mradi wa pamoja ambao mnaufanya wote wanakikundi, mradi huo ndio mtakaouweka kwenye katiba ili kuombea mkopo kupitia wezesha ‘portal’,” anasema Baluwa.

Mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo yanayotolewa na Taasisi ya Mulika, Yusta Awea (22) anasema kutokana na changamoto za kiuchumi alishindwa kumaliza elimu yake ya sekondari na kuishia kidato cha pili hali iliyomlazimu kuungana na mama yake katika biashara ya kuuza chakula.

Anasema kupitia elimu waliyoipata kutoka Mulika, amepata hamasa ya kuinua zaidi biashara yao kupitia fursa za mikopo zinazotolewa na halmashauri. “Baada ya semina tumeunda vikundi na tupo kwenye mchakato wa  kutengeneza katiba ili kupeleka kwa ofisa maendeleo tayari kupata mkopo,” anasema.

“Changamoto iliyopo kwa vijana wengi,” anasema ni kusuasua katika kuchangamkia fursa zilizopo kutokana na kukosa elimu ya namna ya kukamilisha mchakato maombi ya mkopo. “Vijana wengi wanakata tamaa kutokana na mlolongo wa kupata mkopo, lakini elimu ya mara kwa mara na misaada ya kiufundi itawasaidia kuwa na ari ya kujikwamua kiuchumi kupitia mikopo ya halmashauri,” anaeleza.

Awea anasema matamanio yake baada ya kupata mkopo ni kukuza biashara yake ya chakula na nyingine anazotamani kufanya anazoamini zitamuongezea kipato na kuchangia uchumi wa familia na taifa.

Katibu wa Kikundi cha Vijana Wajibika cha Buigiri wilayani Chamwino, Ilumbo Fwejeje anaunga mkono kauli ya Awea kwamba mafunzo ya mara kwa mara kwa vijana yanawasaidia kutambua fursa na kujikwamua kiuchumi kupitia fursa hizo ikiwemo mikopo inayotolewa na serikali.

Fwejeje anayejishughulisha na ushonaji nguo, anasema yeye na wenzake wameunda kikundi kuanzisha biashara ya kuuza vifaa vya ushonaji na ufugaji wa nguruwe. “Tumeandaa katiba na baada ya kuiwasilisha tuliambiwa tumekosea hivyo tulianza kurekebisha ili tuweze kupata mkopo,” anasema.

Anaeleza eneo la biashara ni suala nyeti katika kupata mikopo ya halmashauri kwani moja ya masharti ya kupata mkopo ni kikundi kuwa na eneo la kufanyia shughuli zake linalomilikiwa na wanakikundi na si kuomba maeneo ya watu binafsi kwani hali hiyo itawafanya wakaguzi kuona hiyo ni biashara binafsi na si ya kikundi.

Anasema alipata mafunzo ya ushonaji kutoka kwa Mamlaka ya Elimu na Ufundi Stadi (VETA) na kwamba, anafanya biashara hiyo kwenye eneo la familia. Anasema wakifanikiwa kupata mikopo atahakikisha anakuwa mshonaji mkubwa na mfanyabiashara mkubwa sambamba na kuhakikisha wanarudisha mikopo kwa wakati.

“Tunaomba wadau waendelee kutuelimisha vijana kuhusu uandaaji wa katiba ili tupate mikopo,” anasema. Anaongeza: “Hili ndio eneo linalokatisha tamaa, kwani maofisa maendeleo wanaweza kukurudisha mara kadhaa kurekebisha katiba.”

Aidha, anasema uombaji wa mikopo kielektroniki utasaidia kupunguza gharama za ufuatiliaji wa mikopo katika ofisi za halmashauri. Naye, Magreth Chalo anayejishughulisha na ufugaji wa bata na nguruwe anasema kabla ya kupata
mafunzo hayo hakuwa anafahamu kuhusu mikopo inayotolewa na serikali kwa vijana.

Anasema kabla ya kupatiwa mafunzo hayo, Taasisi ya Maendeleo ya Restless iliwapatia elimu kuhusu umuhimu wa kuunda vikundi na kupeleka andiko lao la biashara kwa ofisa maendeleo.Chalo anasema wanataka kufanya mradi wa ufugaji nguruwe, lakini changamoto inayowakabili ni kukosa eneo la kufanyia shughuli hiyo.

Anasema ufugaji wa nguruwe ‘unalipa’ kwa sababu watu wengi wanawatafuta na kwamba hawana gharama kubwa katika utunzaji.

Mkurugenzi wa Mulika Tanzania, Hussein Melele anasema mradi huo unahakikisha wasichana na vijana wa makundi maalumu wanapewa fursa sawa za kushiriki katika maendeleo ya kiuchumi, hivyo kuimarisha usawa wa kijinsia kwa kusaidia vijana kujiajiri na kuunda biashara endelevu ili kuchochea ajira bora na ukuaji wa uchumi.

Melele anasema mafunzo hayo yanalenga kuwezesha vijana kubuni biashara, kuunganisha vijana na fursa za uchumi, kusaidia usajili wa vikundi na kuhakikisha vijana wanapata mwongozo wa muda mrefu.

“Kupitia mradi huu, vijana wa Dodoma wanawezeshwa kuelewa fursa zilizopo katika wilaya za Bahi, Chamwino, Kondoa, na Dodoma Mjini, ili kuanzisha biashara, kubuni na kuendeleza mawazo ya biashara kwa kuzingatia uhitaji wa soko,” anaeleza.

Anaongeza kuwa, vijana hao hupewa mafunzo ya usimamizi wa fedha, ikiwa ni pamoja na matumizi ya mikopo na huduma za kibenki ili kuendesha biashara zao kwa ufanisi.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *