Vijana kupewa nafasi ushirikiano CCM, Frelimo

DAR ES SALAAM: CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Frelimo cha Msumbiji vimekubaliana kuwashirikisha vijana ili wafahamu uhusiano uliopo kati ya vyama hivyo na kuhakikisha wananchi wa mataifa hayo wanakuwa na uhuru wa kiuchumi.

Pia, vimekubaliana kutengeneza fursa za ajira, hasa kwa kundi la vijana ambalo baada ya kupata elimu kupitia shule na vyuo walivyojenga wanahitaji kuwezeshwa ili wawe na njia zao za kujitegemea.

Akizungumza Dar es Salaam leo, Machi 6, 2026, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira, baada ya kukutana na Katibu Mkuu wa Frelimo, Shakil Aboobacar, katika makao madogo ya chama hicho Lumumba, amesema wamekubaliana kushirikisha vijana kwa kuwa asilimia 65 ya wananchi wa mataifa hayo mawili ni vijana ambao hawaufahamu vizuri uhusiano na mapambano yaliyokuwepo.

“CCM na Frelimo lazima tuwe pamoja katika kutetea maslahi ya nchi zetu na kuhakikisha vijana wanapewa nafasi kubwa katika maendeleo ya mataifa yao. Hilo ndilo jambo kubwa tulilokubaliana,” amesema.

Wasira amesema Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameunda wizara maalum ya kushughulikia changamoto za vijana na kulinda maslahi yao.

“Tumeafikiana kuwashirikisha vijana si tu kwa kuwapa elimu ya kuwaajiriwa, bali pia elimu itakayowawezesha kujitegemea na kujiajiri wenyewe kwa kutumia sayansi na teknolojia,” amesema Wasira.

Amesema vijana wanapaswa kufahamu kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Msumbiji ulijengwa kwa gharama kubwa.

“Tulilipa gharama ya damu. Uhusiano wetu na Msumbiji ni wa damu. Kama kuna uhusiano unaoweza kuandikwa kwa dhahabu, basi huu wetu unaandikwa kwa damu kwa sababu tulishirikiana katika mazingira magumu,” amesema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button