Vijana Queens yapinga kufutiwa matokeo kikapu

KLABU ya mpira wa kikapu ya wanawake, Vijana Queens imetangaza kukata rufaa kupinga kufutiwa matokeo ya mchezo wa nusu fainali ya pili Mkoa wa Dar es Salaam dhidi ya JKT Stars walioshinda kwa pointi 71-58.

Uongozi wa timu hiyo umesema unashughulikia rufaa katika hatua zinazostahili kupata haki.

Advertisement

Mwenyekiti wa Vijana Queens, Eliud Balilemwa amesema:” Tulipokea barua ya kupokonywa ushindi na kuondolewa kucheza fainali. Tumeshafuata taraibu zote za kukata Rufaa kwa mujibu wa kanuni za Ligi ya wanawake Basketball Dar es salaam (BD). Viongozi wa timu wanashugulikia swala hili katika hatua zinazostahili na mtapewa taarifa rasmi.”

“Tuendelee kuwa wavumilivu tukiamini sheria itachukua mkondo wake,”amesema.

SOMA: Vijana Queens yafutiwa matokeo, kisa mchezaji

Kauli hiyo inakuja baada ya Mkurugenzi wa Kamati ya Ufundi na Mashindano wa Chama cha Kikapu mkoa wa Dar es Salaam, Haleluya Kavalambi kutoa taarifa ya timu hiyo kufutiwa matokeo Novemba 1 baada ya kubainika kumchezesha Tupege Lazaro ambaye ameonekana kusajiliwa mara mbili na kucheza ligi mbili tofauti ndani ya msimu mmoja 2024.

Kwa mujibu wa Kavalambi, kamati ya Ufundi imekaa na kujiridhisha kwamba mchezaji Tupege amesajiliwa timu ya Vijana Queens inayocheza ligi ya mkoa wa Dar es salaam msimu wa 2024 na pia amesajiliwa KVZ ya Zanzibar inayocheza ligi ya Unguja msimu wa 2024, hivyo amekiuka kanuni na kifungu namba 17.3.

Mabingwa hao mara tatu mfululizo Ligi Mkoa wa Dar es Salaam haitaendelea na michezo ya nusu fainali ushindi bada ya JKT Stars kupewa ushindi na hivyo, itasuburi kuwania nafasi ya mshindi wa tatu.