TIMU ya wanawake ya Vijana Queens iliyokuwa inashiriki Ligi ya kikapu Mkoa wa Dar es Salaam imefutiwa matokeo ya mchezo wake wa nusu fainali namba 504 ilipocheza dhidi ya JKT Stars.
Taarifa ya Kamati ya Ufundi na Mashindano ya Chama cha Kikapu mkoa wa Dar es Salaam (BD), iliyotolewa na Mkurugenzi wa Ufundi na Mashindano, Haleluya Kavalambi, imetaja sababu ya kufutwa matokea hayo ni baada ya mchezaji wa Vijana Queens, Tupege Lazaro kubanika amesajiliwa mara mbili na kucheza ligi mbili tofauti ndani ya msimu mmoja wa 2024.
Amesema mchezaji huyo amekiuka kanuni zinazosimamia ligi ya mkoa huo inayozuia mchezaji kusajiliwa na timu mbili tofauti na kucheza ligi mbili ndani ya msimu mmoja.
SOMA: JKT Stars, Vijana kuisaka fainali kikapu leo
“Kamati ya Ufundi imekaa na kujiridhisha kwamba mchezaji Tupege Lazaro amesajiliwa timu ya Vijana Queens inayocheza ligi ya mkoa wa Dar es salaam msimu wa 2024 na pia amesajiliwa na timu ya KVZ ya Zanzibar inayocheza ligi ya Unguja msimu wa 2024,”amesema Kavalambi.
Amesema kutokana na kosa hilo mchezaji amekiuka kanuni, kifungu namba 17.3 kinachosema “Kutumia mchezaji aliesajiliwa mara mbili ndani ya msimu mmoja”
“Endapo itagundulika na kuthibika kuwa timu au klabu imemtumia mchezaji kinyume na kifungu hiki itafutiwa matokeo michezo yote aliyocheza mchezaji huyo.
“Mchezaji huyo atafutiwa usajili na hataruhusiwa kucheza msimu husika na kufungiwa kujihusisha na mpira wa kikapu ndani ya nchi kwa mwaka mmoja,”amefafanua na kuongeza kuwa timu hiyo pia, itatozwa faini ya sh 500,000/=
Kufuatia makosa hayo, timu ya Vijana Queens imefutiwa matokeo dhidi ya JKT Stars hivyo imepokonywa ushindi sasa itacheza mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu dhidi ya DB Troncatti.
Katika mchezo wa nusu fainali ya kwanza, Vijana Queens iliifunga JKT Stars kwa pointi 71-58.
Mchezaji Tupege Lazaro amefungiwa kutojihusisha na mpira wa kikapu ndani ya mkoa wa Dar es Salaam kwa muda wa mwaka mmoja na hukumu hiyo imeanza Oktoba 31.
Kwa mujibu wa Kavalambi, Timu ya JKT Stars itacheza michezo ya fainal dhidi ya Don Bosco Lioness.