DAR ES SALAAM: Shirika la Her Initiative kwa kushirikiana na kampuni ya Kazi Connect wameandaa mafunzo ambayo yanawaleta pamoja wahitimu 60 kutoka mikoa tisa na waajiri 25 ili kujenga mahusiano, kufanya mahojiano na kujadili changamoto na maendeleo ya ajira kwa vijana nchini Tanzania.
Mafunzo hayo ya vijana kuajirika (Youth Employability Bootcamp), yanalenga kuongeza ujuzi wa kuajiriwa kwa vijana waliohitimu ili kuongeza nafasi zao za kuajiriwa katika soko la ajira.
Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi wa Her Initiative, Lydia Charles amesema mradi huu unatoa mafunzo, ushauri, na nafasi za wahitimu kujitolea katika maeneo ya kazi.
Pia ameongeza kuwa hadi sasa vijana wamepata mafunzo ya kuandika wasifu wakuvutia, barua ya kazi, ujuzi wa mahojiano, na ujuzi wa kidijitali. Baada ya mafunzo wataunganishwa na washauri na nafasi za kazi ili kupata uzoefu rasmi katika maeneo ya kazi.
“Mafunzo hayo yanakusudia kujenga mahusiano kati ya vijana wanaotafuta ajira na waajiri (Youth Employability Bootcamp) inakusudia pia kuongeza thamani katika ujuzi na fursa ili kujenga vijana wenye shauku na vigezo wanaoweza kuendana na fursa zilizopo katika soko la ajira.”
“Historia ya mradi huu ilianza zamani tulipoanza kuajiri vijana wa kujitolea ambapo tulipokea zaidi ya maombi 200 kila mwaka huku tukiweza kuchukua watu watano pekee”.
Amesema Bootcamp ya mwaka huu ni hatua kubwa mbele, pamoja na ujuzi na nafasi za kujitolea imekuwa ni jukwaa la kuandaa na kujenga mahusiano endelevu kati ya vijana wanaotafuta ajira na wadau wa ajira nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kazi Connect, Gizzel Mbaga, amesema, tunatafutia vijana ajira, Bootcamp tunawaandaa wahitimu ili waendane na soko la ajira kupitia jukwaa la Kazi Connect.
“Ni fursa ya kuhamasisha uongozi wa wanawake vijana katika maeneo ya kazi na ujumuishi wa watu wenye ulemavu katika maeneo ya kazi.”
Winifrida Aluta, mnufaika, amesema kuwa, “mwanzo nilikuwa na wasifu (CV) isiyovutia lakini baada ya mafunzo ya vitendo nimeweza kuboresha wasifu wangu kuwa bora na wenye kueleweka, nimeongeza ujasiri wa mahojiano ya kazi na kupata mbinu zakujibu maswali vizuri kukidhi mahitaji ya waajiri.”