WADAU wa sekta ya kilimo wamepongeza mwito wa serikali kwa vijana wajiajiri kwenye sekta ya kilimo kwa kuwa kinalipa.
Agosti 3 mwaka huu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alihimiza vijana wachangamkie fursa katika mradi uitwao Building a Better Tomorrow (BBT) unaolenga kuongeza ushiriki wa vijana katika kilimo kwa kuwapatia mafunzo, maeneo ya mashamba, mitaji na kuwaunganisha na fursa za masoko.
Majaliwa alisema hayo wakati anauzindua mradi huo katika maonesho ya siku kuu ya wakulima Nanenane kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.
“Vijana wetu fursa ni nyingi nchini kwetu, sekta ya kilimo inabeba fursa zaidi ya asilimia 50, kitendo cha wizara kuzindua mpango mkakati wa vijana kuingia kwenye sekta ya kilimo ni mpango unaolenga kuboresha uchumi wa mto mmoja mmoja kuanzia umri wa vijana,” alisema.
Kwa nyakati tofauti Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji alipokuwa kwenye ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mikoa ya Nyanda za Juu Kusini alisema bilionea wa karne hii atatoka kwenye sekta ya kilimo.
Meneja wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI), kituo cha Hombolo, Dodoma, Dk Joel Meliyo alisema vijana wanahitaji kuandaliwa vizuri ili waelewe wanalima nini, mtaji watapata wapi, watauza wapi na hayo yote yanawezekana kukiwa na utashi wa kisiasa.
“Kwa hakika utashi wa kisiasa ni injini ya mambo mengine kuweza kutokea. Kama kuna utashi hakuna kinachoshundikana. Kutokana na utashi watu wanafika mwezini,” alisema Dk Meliyo.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano cha Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Neema Sitta, alisema anaamini serikali ikiweka mazingira mazuri, vijana wengi watavutika kujiunga kwenye kilimo na nchi itapiga hatua kiuchumi.
Neema alisema vijana wengi wanaohitimu shule na vyuo hawana ardhi kwa kuwa bado inamilikiwa na wazee wao hivyo ni muhimu serikali iangalie namna ya kuwawezesha kwenye hilo.
“Kingine ni matumizi ya teknolojia katika kilimo. Vijana wa sasa huwezi kutegemea wavutike kulima kwa jembe la mkono na hivyo ni muhimu sana kuwawezesha mitaji kwa kuwaunganisha na benki ili walime kwa teknolojia,” alisema.
Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania, Francis Alfred aliunga mkono kuhimiza vijana waingie kwenye kilimo na akasema bodi hiyo imeanzisha kilimo cha mashamba makubwa ya korosho na vijana watapewa maeneo ya ekari tano tano.
“Mwaka huu tumezalisha korosho tani 240,000 na lengo letu ni kufikia tani 700,000 ifikapo mwaka 2026 na hivyo bila kuanzisha mashamba makubwa, kuyaendeleza na kuwapatia vijana itakuwa ngumu kufikisha lengo hilo” alisema Alfred na kuongeza;
“Kwa hiyo kupitia fedha za serikali katika bajeti ya mwaka huu tunasafisha maeneo ya kilimo, tunawapa mbegu za korosho bure na kuwapelekea maofisa ugani. Hizi zote ni fedha za serikali kwa ajili ya kukuza kilimo nchini na vijana ni walengwa wakubwa,”
Mkurugenzi wa kituo cha Tari, Kihinga, mkoani Kigoma kinachojishughulisha na utafiti wa kilimo cha chikichi, Dk Filson Kagimbo alisema vijana wanapoingia kwenye kilimo wasifikirie kupata fedha za haraka haraka.
Meneja Mawasiliano wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), Amani Nkurlu, alisema kilimo kina tija kuliko kazi nyingi za kuajiriwa hivyo vijana wabadili mtazamo na waipende sekta hiyo.
“Vijana wengi wana mtazamo finyu wa kumaliza kozi zao, kupata kazi ya ofisini, kupanga chumba na kuingia kazini kuanzia saa mbili asubuhi na kutoka saa 11. Lakini ukweli kwenye kilimo wanaweza kupiga hatua kubwa sana na hivyo kinachotakiwa ni kuwabadilisha mtazamo,” alisema.
Ofisa Masoko wa Kampuni ya Kuzalisha Mbegu ya Beula Seeds Co & Cons Limited, Evaristo Mbwaga alisema vijana wakilima kisasa sekta hiyo itawalipa lakini ni muhimu wawezeshwe mitaji.
“Kilimo cha kisasa hakiwezekani bila kupata mitaji. Lakini kwa matamshi ya Waziri Mkuu ninaamini benki zitafanya urahisi wa mikopo kwa wakulima na riba nafuu, hususani vijana,” alisema Mbwaga.