Vijana washauriwa kuwasilisha bunifu zao kujiwekeza

DAR ES SALAAM: VIJANA ambao wanamiliki kampuni changa wameshauriwa kuwasilisha mawazo yao ya ubunifu, ili kuendelea kujiimarisha kwenye uwekezaji.

Akizungumza jana, Rodrique Msechu, mwanzilishi wa kampuni ya Serengeti Business Angels Network, alisema lengo ni kuwapa wawekezaji fursa ya kufanya nao biashara na uwekezaji.

“Wito wangu kwa vijana, wajaribu kujitolea kwenye kampuni kama hizi, utajifunza mambo mengi, namna ya kuzungumza na wawakezaji,” amesema Msechu.

Aidha, kupitia shindano hilo, kampuni za kidijitali zimeendelea kujiimairisha kuichumi, hali itakayowatia moyo waajiriwa wake, kufuatia kutumia fursa mbalimbali zinazoendelea kuibuka nchini.

Hatua hiyo inafanya kampuni changa kuendelea kuimarisha uwekezaji wake kwa kutumia fursa hizo ikiwemo kuwasilisha wazo la ubunifu linalowezesha mawakala wa huduma za fedha kwa njia ya simu kupanua huduma zao.

Flowteller ni kampuni ambayo imetumia kwa ufanisi wazo hilo na kushinda Sh milioni 1.8 katika toleo la 11 la Harambee Evening lililofanyika Dar es Salaam.


Kampuni hiyo ilishinda kiasi hicho cha fedha kwa kuzishinda kampuni za Lipisha na Winvo, katika mashindano hayo yaliyoandaliwa na kampuni ya Serengeti Angels na WakaPay na Ubalozi wa Uholanzi.

Akizungumza baada ya ushindi huo, mwanzilishi wa Flowteller David Bwire alisema wanafurahi kuona wazo lao limefanikiwa na kuthibitisha uwezo wa timu yao katika ubunifu wa teknolojia.

Alieleza kuwa teknolojia ya Flowteller inawawezesha wafanyabiashara kutoa huduma mbalimbali za kidijitali moja kwa moja kwa jamii inayowazunguka.

Kwa upande wa Lipisha, waliwasilisha jukwaa la malipo ya biashara kwa biashara (B2B) pamoja na mfumo wa kusaidia kampuni kufuatilia na kusimamia miamala yao kwa ufanisi zaidi.

Nayo Winvo ilitambulisha suluhisho la kufadhili maagizo ya manunuzi ya ndani (LPO) kupitia mfumo wa uchangiaji wa fedha kutoka kwa wawekezaji (peer-to-peer crowdfunding), hatua inayolenga kusaidia biashara ndogo na za kati kupata mtaji wa kuendesha shughuli zao.

Katika hafla hiyo, waandaaji pia walitoa ufafanuzi kuhusu WakaPay, kampuni ya teknolojia ya fedha inayowezesha watumiaji wa huduma za fedha kwa simu nchini Tanzania kulipa wafanyabiashara nchini Kenya moja kwa moja.

Mfumo huo unaruhusu malipo ya kuvuka mipaka kwa viwango shindani vya ubadilishaji fedha na ada ya dola moja kwa miamala isiyozidi shilingi 150,000, huku miamala inayozidi kiwango hicho ikitozwa asilimia 1.5.

Mwanzilishi wa WakaPay George Mtemahanji alisema huduma hiyo inalenga kurahisisha miamala ya kifedha kati ya nchi za Afrika wakati biashara za kikanda zikiendelea kukua.

Kwa upande wake mshiriki wa hafla hiyo, mshauri wa masuala ya mali isiyohamishika Wilma Mallya, alisema alivutiwa na kiwango cha ubunifu kilichoonyeshwa na washindani wote watatu Flowteller, Lipisha na Winvo.

Waandaaji wa tukio hilo walisema mpango wa Harambee Evening unaendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Serengeti Angels, WakaPay na Ubalozi wa Uholanzi katika kukuza ujasiriamali na kuendeleza mfumo wa kampuni changa za teknolojia nchini.

Harambee Evening ni jukwaa linaloendeshwa na jamii ya wajasiriamali, linalolenga kutoa fursa kwa kampuni changa kuwasilisha mawazo yao, kupata umaarufu pamoja na kuunganishwa na wawekezaji na wadau mbalimbali wa biashara.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button