Vijana wataka amani ilindwe

TANZANIA ina jumla ya vijana zaidi ya milioni 21 wenye umri kati ya miaka 15 hadi 35, sawa na takribani asilimia 34.5 ya Watanzania wote, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.
Takwimu hizi zinaonyesha wazi kuwa vijana ndio kundi kubwa la wananchi na nguvu kazi kuu inayobeba mustakabali wa taifa. Aidha, tafiti za nguvu kazi zinaonesha kuwa zaidi ya nusu ya nguvu kazi nchini ni vijana, jambo linalothibitisha nafasi yao muhimu katika maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Katika mazingira hayo, wataalamu na wadau mbalimbali wanaeleza kuwa uwekezaji kwa vijana si chaguo bali ni lazima, hasa katika sekta za elimu, ajira, teknolojia na ujasiriamali. Kwa sasa, vijana wengi nchini Tanzania wanapata fursa katika maeneo mbalimbali ikiwemo sekta ya biashara, viwanda, teknolojia ya kidijitali na kilimo cha kisasa. Serikali pia imeendelea kuweka mazingira wezeshi kupitia sera na mipango inayolenga kuwajengea vijana ujuzi na mitaji ya kujiendeleza.
Hata hivyo, pamoja na fursa hizo, bado vijana wengi wanakabiliwa na changamoto kama ukosefu wa ajira rasmi, hali inayowasukuma wengi kujikita katika sekta isiyo rasmi na ujasiriamali mdogo. Ni katika muktadha huo ambapo wito wa kulinda amani umeendelea kusisitizwa, hususan kwa vijana ambao ndio waathirika wakubwa wa vurugu na migogoro.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Dailynews Digital, Waziri wa Wanafunzi anayeshughulikia masuala ya usalama, Benedict Lubimbi, amesema anashangazwa na watu wanaojaribu kuharibu taswira ya vijana huku wakisahau kuwa ndio tegemeo la taifa. “Ukiangalia kwa karibu sana, vijana ndio nguvu kazi ya taifa inayotegemewa. Ni kundi muhimu sana, hasa wakati wazee wanapoondoka,” alisema Lubimbi.
Amesisitiza kuwa maendeleo ya Tanzania yanategemea uwajibikaji wa kila mwananchi katika kudumisha amani, upendo na mshikamano, akimnukuu Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere, aliyesema: “Umoja wa kitaifa ndio msingi wa utulivu na ustawi wa nchi yetu.”
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Wanafunzi wa chuo hicho, Zairudin Ismaily Haifi, amesema kuwa amani ya nchi haiwezi kupatikana bila utulivu wa jamii, huku vijana wakiwa mstari wa mbele katika kulinda hali hiyo. “Sisi kama vijana tuna mchango mkubwa sana katika kulinda amani. Vijana ni nguvu kazi ya taifa, hivyo tunapaswa kuimarisha amani,” alisema.
Ameongeza kuwa uwepo wa amani hupunguza chuki katika jamii na kuimarisha uhusiano kati ya wananchi na serikali. Wanafunzi wa fani ya Sayansi ya Jamii walieleza kuwa ipo haja ya kuendelea kuwaelimisha vijana kuhusu umuhimu wa amani ili kujenga uzalendo na kuhakikisha wanakuwa walinzi wa taifa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Mwanafunzi wa mwaka wa kwanza, Given Fadhil, amesema kuwa taifa linahitaji watu wenye upendo na umoja ili kuondoa migogoro inayoweza kuvuruga amani. “Nchi yoyote inahitaji watu wenye upendo na umoja. Hii husaidia kuondoa sintofahamu zinazoweza kuvuruga amani ya nchi,” alisema.
Ameongeza kuwa kuheshimiana na kulinda haki za binadamu ni msingi muhimu wa mshikamano wa kitaifa, huku akionya kuwa migawanyiko inaweza kusababisha vurugu na machafuko. SOMA: Mangu aonya uvunjifu wa amani
Naye Jamilla Kimbo, mwanafunzi wa fani ya sayansi ya mazingira, amesema kuwa amani ina mchango mkubwa katika ustawi wa vijana kwani huwapatia mazingira salama ya kupata elimu, ajira na fursa nyingine za maendeleo. “Katika nchi yenye amani, vijana ndio wanufaika wakubwa kupitia elimu bora, usalama wa maisha na fursa za ajira,” alisema.
Ongezeko hili la kundi la vijana zaidi ya milioni 21 linaweza kuwa chachu kubwa ya maendeleo ikiwa litaongozwa na kuangaliwa vizuri, kwa kutambua kulinda amani ni msingi wa kuhakikisha fursa hizo zinawanufaisha vijana na taifa kwa ujumla.




thisis a fantastic article, really nice created, i enjoy reading it, i will be back to check out for latest update, keep up the good work and applause. usa.yandaz.com