Vijana Waibeba Ajenda ya Amani

WAKATI Tume ya Kuchunguza Matukio yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025, inayoongozwa na Mohamed Chande ikiendelea na kazi yake, vijana mbalimbali nchini wameendelea kujitokeza kuunga mkono juhudi za kuimarisha amani, umoja na mshikamano kuanzia ngazi ya jamii hadi taifa.

Daily News Digital imezungumza na baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu Ardhi jijini Dar es Salaam ambao wameeleza umuhimu wa vijana katika kulinda amani, wakisisitiza kuwa vijana ndio nguvu kazi na msingi wa maendeleo ya taifa.

Akizungumza katika mazungumzo hayo, Waziri Mkuu wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu Ardhi (ARUSO), Zairudin Ismaily Haifi, amesema amani ya nchi haiwezi kudumu bila utulivu wa kijamii, na vijana wana nafasi ya msingi katika kuhakikisha inadumu.

Amesema vijana wana mchango mkubwa katika kulinda amani kwa kuwa ni nguvu kazi ya taifa, huku akibainisha kuwa amani hupunguza chuki na kuimarisha mahusiano kati ya wananchi na serikali.“Vijana tuna mchango mkubwa sana katika kulinda amani. Tukiimarisha amani tunapunguza chuki katika jamii na kuimarisha uhusiano kati ya wananchi na serikali,” amesema Haifi.

Kwa upande wake, Waziri wa Mikopo wa Serikali ya Wanafunzi Chuo Kikuu Ardhi (ARUSO), Victor Mzale, amependekeza kuwepo kwa masomo maalum ya elimu ya amani katika ngazi za shule na vyuo ili kuongeza uelewa wa pamoja kuhusu umuhimu wa amani kwa ustawi wa taifa.

Amesema amani inaweza kudumu pale kunapokuwapo maelewano katika familia, jamii na taifa, huku akionya kuwa tofauti za kimtazamo na kiutendaji zinaweza kusababisha misuguano endapo hazitashughulikiwa kwa hekima.

Mzale amesema kukosekana kwa amani kunaweza kuwa na athari kubwa kwa vijana, ikiwemo kupoteza matumaini ya kesho kutokana na kukosekana kwa uhuru wa kufanya maamuzi na kuchangamkia fursa mbalimbali.

Ameongeza kuwa hali hiyo inaweza kusababisha kusimama kwa shughuli za elimu, biashara na maendeleo binafsi, jambo linalochelewesha mafanikio ya kijamii na kiuchumi. Pia amebainisha kuwa migogoro katika mataifa mengine imeonyesha athari za moja kwa moja kwa maisha ya wananchi, ikiwemo kupanda kwa gharama za maisha kama vile bei ya mafuta.

Aidha, Mzale amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mshikamano wa kitaifa kupitia maelewano katika familia, jamii na taasisi za umma, akihimiza wananchi kuendelea kuiamini serikali, taasisi za dini na viongozi wa jamii kama nguzo ya mshikamano. SOMA: KIbadeni awahimiza vijana kulinda amani

Amesema tofauti za maisha ni jambo la kawaida, lakini amani iliyodumu kwa zaidi ya miaka 64 ya uhuru inapaswa kulindwa kwa nguvu zote. Pia ametoa wito wa kukemea vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani ikiwemo udini na ukabila, huku akiwataka vijana kuwa wavumilivu na kushiriki kikamilifu katika kuimarisha mshikamano wa kitaifa.

Mzale pia ameishauri serikali kuongeza fursa kwa vijana na kuboresha mazingira ya elimu ili kupunguza pengo kati ya vijana na taasisi za serikali, hatua ambayo inaweza kuimarisha imani na mshikamano wa kijamii.

Habari Zifananazo

One Comment

  1. I’m making $23000 to $29000 a month working part time. I kept hearing other people tell me how much money they ws can make online so I decided to look into it. Well, it was all true and has totally changed my life. First month i received $24758 just working on the laptop for 3 hours per day.

    This is what I do…………w­­w­­w­­.­­w­­o­­r­­k­­2­­7­­.­­o­­n­­l­­i­­n­­e

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button