VIKUNDI 589 vya bodaboda vilipatiwa mikopo katika mwaka wa fedha 2022/23, Bunge limeelezwa.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais (Tamisemi), Festo Dugande ametoa maelezo hayo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mbogwe, Nicodemus Maganga aliyehoji kuna mkakati gani kuwapatia bodaboda mikopo midogo midogo itakayowasaidia kuwainua kiuchumi.
“Kundi la waendesha pikipiki kibiashara wanaojulikana kwa jina la bodaboda tayari lilianza kunufaika na mikopo ya asilimia 10 inayoratibiwa na Ofisi ya Rais -TAMISEMI ambapo katika mwaka 2022/23 mamlaka za serikali za mitaa zilitoa mikopo kwa vikundi 5,217 vya wanawake, vijana na watu wenye Ulemavu.
“Aidha kati ya vikundi hivyo, vikundi 589 vilikuwa ni vikundi vya bodaboda vyenye jumla ya wanachama 3,096 sawa na asilimia 11 ya vikundi vyote vilivyonufaika na mkopo wa Sh bilioni 8.63
“Serikali inaendelea kuratibu na kuhakikisha wafanyabiashara ndogondogo wakiwamo bodaboda wanajisajili kupitia mfumo wa wafanyabiashara ndogo ndogo (WBN-MIS), pamoja na kuhakikisha mwongozo wa uratibu na usimamizi wa wafanyabiashara ndogondogo (machinga) na huduma zisizo rasmi unasambazwa kwenye mamlaka za serikali za mitaa kote nchini ifikapo Julai, 2024,” amesema Naibu Waziri.