Viongozi CCM Iringa wanolewa udereva

KATIKA kuadhimisha miaka 30 ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na nusu karne ya elimu ya ufundi stadi nchini, viongozi wakuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Iringa walikuwa miongoni mwa madereva zaidi ya 100 walioshiriki mafunzo maalum ya udereva wa malori na mabasi.

Miongoni mwa viongozi hao ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daudi Yasin, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (MNEC) Salim Asas, na Katibu wa CCM Mkoa, Said Goha.

Mafunzo hayo ya muda mfupi yalilenga kuwajengea madereva ujuzi na uelewa wa kina kuhusu sheria za usalama barabarani, kwa lengo la kupunguza ajali na kuboresha utendaji wao barabarani.

Mkuu wa Chuo cha Ufundi Stadi VETA Iringa, Mwalimu Pasiens Nazareth Nyoni, alisema chuo hicho kina uwezo wa kufundisha madereva 500 kwa mwezi, na kinaendelea kupanua miundombinu ili kuboresha zaidi mafunzo hayo.

“Tunawakaribisha wale wote waliopata ujuzi wa udereva kwa njia isiyo rasmi kuja VETA ili warasimishwe kupitia mfumo wa mafunzo rasmi na kupata vyeti vitakavyowawezesha kupata ajira,” alisema Nyoni.

Aidha, alifafanua kuwa mafanikio ya VETA Iringa yanaonekana wazi kupitia ongezeko la fani zinazotolewa chuoni hapo, kutoka fani nne hadi 12 kwa sasa, hali inayopanua fursa za ajira kwa vijana.

Baada ya kuhitimu mafunzo hayo ya mwezi mmoja, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daudi Yasin, alisema elimu hiyo imewawezesha kuelewa kwa undani sheria mpya za barabarani na umuhimu wa kuziheshimu ili kusaidia kupunguza ajali.

“Nichukue fursa hii kuipongeza pia VETA kwa juhudi zake kubwa za kuwaandaa vijana kuwa na ujuzi wa fani mbalimbali zinazowawezesha kujiajiri. VETA mnaisaidia kwa kiwango kikubwa serikali ya CCM kutekeleza Ilani yake kwa vitendo,” alisema.

Naye, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Salim Asas, alisisitiza kuwa licha ya madereva wengi kuwa na uzoefu wa muda mrefu, bado kuna umuhimu wa kujifunza upya kutokana na mabadiliko ya sheria za barabarani na ongezeko la vyombo vya usafiri kama bajaji na bodaboda.

“Kuna ongezeko kubwa la magari makubwa, na changamoto mbalimbali za usalama barabarani zinahitaji madereva waliopata mafunzo sahihi. Tunaishukuru VETA kwa kutupa fursa ya kushiriki,” alisema Asas.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa (RPC), Allan Bukumbi, alikipongeza chuo hicho kwa mchango wake katika kuimarisha usalama barabarani kupitia mafunzo ya udereva.

Alisema zaidi ya askari 90 wa Jeshi la Polisi wamepata mafunzo kama hayo, hatua inayosaidia katika kudhibiti ajali za barabarani.

“Udereva ni taaluma inayohitaji nidhamu na weledi. Tunapaswa kuwa waangalifu, kusikiliza mafunzo na kuhakikisha tunazingatia sheria za usalama barabarani,” alisema RPC Bukumbi.

Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Suzan Magani, alieleza kuwa wakati mamlaka hiyo inaanza kazi, mikoa ya Iringa, Njombe, na Ruvuma ilikuwa na vyuo viwili pekee vya ufundi.

Hata hivyo alisema, kwa sasa idadi hiyo imeongezeka hadi vyuo nane, huku chuo kipya cha VETA Ludewa kikijengwa ili kukidhi mahitaji ya soko la ajira na miradi inayoendelea wilayani humo.

Naye, Mratibu wa Mafunzo wa VETA Iringa, Edmund Enugu, alisema kuwa pamoja na madereva wengi kuwa na leseni, wanapaswa kupata mafunzo ya mara kwa mara ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia za magari.

Katika sekta nyingine, Sara Joseph, mwanafunzi wa fani ya uchomeleaji vyuma chuoni hapo, alisema kuwa mafunzo anayoyapata VETA yatamsaidia kujiajiri na kuepuka changamoto za kutafuta ajira.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button