MAREKANI : VIONGOZI mbalimbali duniani wamempongeza mgombea wa chama cha Republican, Donald Trump alipotangazwa kuwa mshindi katika uchaguzi wa rais wa Marekani.
Miongoni mwa viongozi waliompongeza Donald Trump ni Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer ambaye amesema ataendelea kushirikiana na Marekani kwa ukaribu, “ni ushindi wa kihistoria”, alisema Starmer.
Kiongozi mwingine, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameelezea utayari wake wa kufanya kazi na Donald Trump. “Hongera Trump,tuko tayari kufanya kazi pamoja kama tulivyofanya kwa miaka minne, kwa amani na ustawi zaidi.” Alisema Macron
Viongozi wengine waliotuma salama za pongezi ni Rais wa Tume ya Muungano wa Ulaya Ursula von der Leyen ambaye amesisitizia umuhimu wa mahusiano ya Umoja wa Ulaya na Marekani.
Naye Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz akisisitiza umuhimu wa kufanya kazi na Marekani kwa lengo la kukuza ustawi wa mataifa mawili kati ya Marekani na Ujerumani.
Huku Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amemuelezea Donald Trump kama rafiki na kuonyesha matumaini yake ya kuendelea kukuza uhusiano kati ya Uturuki na Marekani.
Kwa upande wake Mfalme Abdullah II wa Jordan amesema serikali yake itaendelea kushirikiana na Marekani katika kuimarisha amani na utulivu wa kikanda na kimataifa.
Wengine waliotoa salamu za pongezi, Rais wa Misri Abdel Fattah el-Sisi yeye amesema yuko tayari kufanya kazi na Marekani pamoja na kuleta amani na utulivu katika Mashariki ya Kati.
Emir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, atahakikisha anaimarisha uhusiano wa kimkakati utakaokuza usalama na utulivu katika kanda ya ulimwengu.