WAGOMBEA wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA ) katika vitongoji na vijiji vya Kata ya Mikese , Wilaya ya Morogoro wameomba wananchi kuendelea kudumisha amani na utulivu uliopo wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi wa Serikali Za Mitaa kesho.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika kijiji cha Fulwe , Kata ya Mikese, Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kwenye kuhitimisha kampeni zilizodumu siku zaidi ya nane ,mgombea wa Mwenyekiti Kitongoji cha Dindili, Bernald Tambala pamoja na Rehema Dega Siari wa Kitongoji cha Ukomanga kwa nyakati tofauti walisema kampeni zilifanyika kwa amani.
Waliwaomba wananchi waliojiandikisha hasa wa vitongoji hivyo na vingine ambavyo vina wagombea wa chama chao wajitokeze kwenda kupinga kura na kuwachangua ili waweze kuwaongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Mgombea Rehema amesema Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akiwajali wananchi kwa serikali yake kuleta fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa zananati na maji lakini viongozi waliopo madarakani kwenye kijiji na kitongoji wamekuwa wakimwangusha kwa kutafuna fedha za miradi na wao wakichanguliwa wanasimamia miradi hiyo.
Kwa upande wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Morogoro Vijijini kimeeleza matarajio ni kupata ushindi mkubwa katika vijiji vyote 149 na vitogoji 734 licha ya vyama vya upinzani kusimamisha wagombea kwenye takribani vijiji 20.
Mwenyekiti wa CCM wilaya hiyo ,Gerold Mlenge amesema hayo wakati akihitimisha kampeni katika kijiji cha Fulwe ,kata ya Mikese ambapo alishukuru kumalizika kwa usalama na kisisitiza wananchi waliojiandikisha wajitokeza Novemba 27, mwaka kutumia haki yao ya kidemokrasia ya kupinga kura na kuwachangua wagombea wa chama hicho.
“ Tumehitimisha kampeni kwa amani na utulivu tangu tulipozindua eneo la Kijiji cha Bwakila Chini katika Kata ya Dhutumi na kuhitimishwa katika Kijiji cha Fulwe, kata ya Mikese na nimatarajio yangu uchaguzi utakuwa na amani na hata baada ya kuchaguzi huu” amesema Mlenge.