Viongozi wa dini wakemea ndoa za jinsi moja

Dk Alex Malasusa

KATIKA kusheherekea Sikukuu ya Pasaka jana, viongozi wa dini ya Kikristo katika maeneo mbalimbali nchini wameitaka jamii kuachana na visasi, kudumisha upendo huku suala la kupinga ndoa za jinsia moja likionekana kugusa mahubiri mengi.

Miongoni mwa viongozi hao ni Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Yakobo Mkuu Mtume Kijitonyama, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Novatus Mbuya ambaye kwenye Ibada ya Misa Takatifu ya Pasaka aliwataka Wakristo na Watanzania kwa ujumla kuwa makini na kujiepusha na mambo yaliyo kinyume na Mungu vikiwemo vitendo vya ndoa za jinsia moja kwa kuwa hiyo ni laana.

Alisema kupitia mitandao ya kijamii, watu wamejikuta wakikumbatia mambo yasiyofaa yakiwemo masuala ya ndoa ya jinsia moja.

Advertisement

“Mwanaume au mwanamke ameumbwa awe hivyo, hivyo jivunie uanaume wako na uanawake wako, leo imefikia mahali mwanaume anataka aolewe, atembee na mwanaume mwenzake, ni mambo ya laana, hayana baraka katika maisha,” alisema.

Aliongeza: “Ni majanga ya kitaifa na vizazi vyetu tunaviharibu, tamaa hizi ni za kifo, hata wanyama na ndege hawafanyi hivi, haya siyo mambo ya kuchekea, ni majanga katika jamii yetu.”

Kutokana na hali hiyo, aliwataka Wakristo na wasio Wakristo kufanya toba na kuenenda kama Mwenyezi Mungu alivyowaumba na kuishi kama waafrika badala ya kuiga au kurudi kwenye enzi za Sodoma na Gomora.

Kwa upande wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), limetaka jamii kuacha kuhalalisha dhambi kwa kujificha katika kivuli cha haki za binadamu huku likikemea ndoa za jinsia moja lililoonekana kushika kasi siku za karibuni, kutokana na kuporomoka kwa maadili.

Hayo yalisemwa na Askofu wa kanisa hilo Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa alipokuwa akihubiri kwenye ibada ya maadhimisho ya Sikukuu ya Kufufuka Yesu Kristo (Pasaka) iliyofanyika katika kanisa la KKKT usharika wa Azania Front, Dar es Salaam.

Alisema katika dhana ya haki za binadamu watu wameamua kumsahihisha Mungu katika suala la uumbaji alipoamua kuwaumba mwanamke na mwanaume ili kuendeleza uumbaji wake na kuamua kushabikia ndoa za jinsia moja.

“Ndugu zangu hakuna asiyejua dunia sasa hivi inakokwenda, wanakotaka hata kubadilisha mpango wa Mungu katika uumbaji, ninyi ni mashahidi tulipoanza miaka hii ya 2000 kukawa na majadiliano makubwa yaliyokuwa yakisukumwa kwa nguvu sana juu ya ndoa za jinsia moja, lakini yalishtua zaidi si kwamba hayakuwepo, hata biblia inatuambia wakati wa sodoma na gomora yalikuwepo lakini yalianza kustua zaidi yalipoingia mpaka kwenye kanisa,” aliongeza.

“Watu kusema hebu tuwape haki wanadamu, Mungu haonekani sasa hivi lakini najaribu kupiga picha kwamba Mungu anatuangaliaje sisi wanadamu ambao tunajaribu hata kufikirifikiri kwamba pengine inawezekana, Mungu katika neno lake aliweka utaratibu kwamba uumbaji wake utaendelezwa kwa mwanaume na mwanamke,“ alisema.

Alisema mwaka 2010 KKKT ilitoa tamko kupinga uhusiano na ndoa za jinsia moja na hata sasa halikubaliani na linakemea na linataka wakristo wote wajue kwamba kanisa limekemea ndoa za jinisia moja na kwa uumbaji wa Mungu ndoa anazozifahamu ni za mwanaume na mwanamke pekee.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Mennonite Tanzania, Nelson Kisare katika ibada maalumu ya kusherehekea Pasaka, iliyofanyika katika kanisa hilo Upanga, Dar es Salaaam alisema kanisa lake linapinga suala la mapenzi ya jinsia moja na kuitaka jamii kuungana kwa pamoja kutoa elimu ya dini katika mwendelezo wa kupinga suala hilo.

Aidha, aliupongeza uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitahada za kuhakikisha wanatokomeza suala la rushwa ambayo aliita kuwa ni adui wa haki na kwamba kwenye rushwa hakuna amani. Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Kanisa la Mennonite Tanzania, Amos Masanja alisema kuwa katika kusherehekea siku ya Pasaka jamii haipaswi kufanya matendo kinyume na sheria za mungu, bali kwa pamoja waungane kutenda mema.

Askofu Jimbo Katoliki la Tunduru Masasi, Mhashamu Filbert Mhasi ametaka wazazi kuwachunguza watoto wao na kujua mambo gani wanayafanya mahali popote wanapokuwa na wasiwaache warukie kila kitu kwa sababu jamii kwa sasa ina mambo mengi ya hovyo kupitia katika mitandao.

Alisema hayo jana wakati akitoa ujumbe wa Pasaka kwa waumini wa Kikristo Tanzania kwenye Misa ya Pasaka kitaifa iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Francis Exavery Tunduru mkoani Ruvuma. Sambamba na hilo ametaka wazazi kuhakikisha usalama wa watoto wakati wa likizo hata kama wanawapeleka kwa ndugu wa karibu kama mjomba, shangazi, baba mdogo au mama mkubwa wajiulize kuhusu usalama wa watoto mahali wanapowapeleka ukoje.

Alisema watoto wengi wanaharibika kutokana na wazazi na walezi kuacha mitandao ya kijamii kuwalea na kuwafundisha watoto kitu kinachowakutanisha watoto na mambo mengi ya kutisha ikilinganishwa na umri wao. “Tuwalee watoto waisikie sauti ya Mungu kwanza kwani watathamini na kujali utu wa mwanadamu. Tuwafanye waweze kufanya maamuzi mazuri katika maisha yao,” alisema.

Aidha, Askofu Mhasi aliwataka vijana kutoendekeza mafanikio kwa njia ya mkato katika maisha kwani inawaingiza vijana wengi katika hatari na kuishia kudanganywa na kusababisha kuangukia katika makundi ya hovyo. Askofu Mhasi aliwausia waumini wa Kikristo kuamini katika nguvu ya upendo na neno la Mungu na kuacha tabia ya kulipa kisasi kwa sababu kisasi hakijengi badala yake kinabomoa familia.

Naye Askofu msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Stefano Musomba, amewataka wakristo na watu wengine kutambua kuwa ulimwengu wa sasa umeathiriwa na mila ya kifo kutokana na matukio ya kutisha yakiwemo mauaji, vita, ushirikina, rushwa na ulafi wa madaraka. Aliongeza”Tunaharibu watoto wetu kwa nyimbo na michezo ya ajabu, leo watoto wapo peke yao wanalelewa na ulimwengu, tunawapa simu na wanaangalia picha za ajabu, utandawazi unatupotosha, watoto wa kiume wanataka kulelewa, wamekuwa wavivu, malezi hayana tena mizizi, hatulei watoto vizuri.”

Askofu Mstaafu wa Jimbo Katoliki Morogoro, Telesphor Mkude amewataka Watanzania kusimamia misingi imara ya maadili mema, mila na desturi nzuri zilizopo ili kujenga taifa lenye kumcha Mungu. Askofu Mstaafu Mkude alitioa rai hiyo wakati wa mahubiri ya Ibada ya Misa Takatifu ya Jumapili ya Pasaka kwa waumini wa kanisa hilo ambayo ilifanyika katika Kanisa kuu la Mtakatifu Patrice mjini Morogoro.

Hivyo aliisihi jamii kuacha kuchanganya mila na desturi ambazo hazifai katika taifa na pia zinakwenda kunyume kwa kumcha Mwenyezi Mungu.

Imeandikwa na: John Nditi (Morogoro), Matern Kayera, Selemani Nzaro, Anna Mwikola, Rehema Lugono, Rahim Fadhili (Dar)

 

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *