VIONGOZI wa dini mkoani Tanga wameishauri serikali kuweka siku maalum ya kuliombea taifa wakati huu kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili taifa liendelee kubaki salama.
Ombi hilo wamelitoa mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batlida Buriani alipokutana na viongozi hao ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuongeza hamasa ya uandikishaji wananchi katika daftari la wapiga kura.
Akizungumza leo Oktoba 19, 2024 Mwenyekiti wa Kamati ya Amani mkoani hapa, Shekhe Ali Luuchu amesema kuwa taifa ambalo lipo mikononi mwa maombi ya viongozi wa dini ni salama hivyo wanaimani maombi Yao yataweza kukubaliwa.
“Tunaishukuru serikali yetu ni sikivu mara kwamara imekuwa ikikutana na viongozi wa dini Kwa ajili ya kupata maoni yao na Rai kuhusiana na mambo mbalimbali ya kuleta maendeleo kwenye taifa hili,”amesema mwenyekiti huyo.
Mchungaji Elizabeth Bayo amesema kuwa ushiriki wa viongozi wa dini unakuja wakati huu hamasa ya uandikishaji wananchi katika daftari la wakazi ni kubwa ambayo imefika hadi katika makazi ya watu.
SOMA: Serikali, viongozi wa dini kushirikiana
Kwa upande wake Shekhe wa Wilaya ya Pangani, Zubeir Nondo ameiomba serikali katika kipindi hiki kilichobaki kusogeza huduma ya uandikishaji katika taasisi za dini ambazo nyingi zina watu ambao tayari wamefikisha umri wa kushiriki kwenye uchaguzi Ili kuongeza zaidi ya watu walioandikishwa.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dk Batlida Buriani amewaomba viongozi hao wa dini kuendelea kutoa hamasa Kwa waumini wao kuweza kushiriki kwenye zoezi la uandikishaji Ili waweze kushiriki kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa.