Viongozi wa Yanga Bukoba, wanachama hawataki tena dabi

VIONGOZI, wadau na mashabiki wa timu ya Yanga Tawi la Bukoba mkoani Kagera wamekutana kuunga mkono kauli ya Kamati ya Utendaji ya timu hiyo kuwa hawatacheza tena mechi dhidi ya Simba.
Mchezo huo wa Ligi Kuu namba 184 ulipaswa kuchezwa Machi 8, 2025 lakini haukufanyika kutokana na Simba SC kugomea baada ya taarifa ya kuzuiwa kufanya mazoezi na mabaunsa wa Yanga siku moja kabla ya mechi uwanja wa Mkapa.

Katibu wa Matawi ya Yanga mkoani Kagera Jamali Kalumuna aliwaongoza wadau kufungua kikao cha kutoa kauli ya pamoja kuwa hawataki tena mchezo wa marudiano badala yake wanaiomba Bodi ya Ligi Kuu na TFF kuwapatia Yanga pointi 3 na goli 3 kwa mujibu wa kanuni.
“Kwanza kabisa tunaungana na kamati tendaji kupitia kwa Rais wa Yanga injinia Hersi kuwa kwa pamoja matawi yote ya Mkoa wa Kagera hatutacheza tunachohitaji ni kupatiwa pointi zetu na magoli yetu matatu kwa sababu kuahirishwa kwa mchezo huo hakukufata kanuni,”amesema Kalumuna.

Peter Matete, Mjumbe wa Tawi la Yanga Bukoba amesema ni vyema kanuni zikazingatiwa ambapo ameongeza kuwa sio salama kwa maswala ya mpira kufuata busara na kushauri kuwa timu yoyote isipofuata kanuni bila kujali ukubwa wa Timu ikatwe point na hiyo itasaidia kuweka heshima ya mpira nchini na kupandisha hadhi ya ligi ya Tanzania.
Ezra Festo mwanachama wa Yanga mkoani Kagera amesema kuwa ni aibu na kukosa kuwajibika endapo busara zinaendekezwa na kufuta kanuni za ligi na kuumiza hisia za watanzania ambao ndio wadau wakubwa wa mpira wa miguu huku akidai kuwa kwa mara ya kwanza viongozi wa Bodi ya Ligi wanapaswa kuwajibika kwa kuumiza hisia za mashabiki walitoka ndani ya nchi na nje ya nchi kuja kushuhudia mchezo huo.

Gozbeth Kamuntu mwanachama wa Yanga amesema ndapo Yanga hawatapata haki ya kupata point 3 na magoli 3 kikanuni mashabiki wa Yanga na wanachama kutoka mkoani Kagera watafanya maandamano ya amani kutoka Bukoba hadi Dar es salaam kudai point za Yanga ambapo amedai kuwa kauli ni ile ile kuwa hawachezi.
Sharifu Hasan shabiki wa timu ya Yanga amesema kuwa siku hiyo alisafiri kutoka mkoani Kagera kwenda Dar esa Salaam na alilipa tiketi yake kushuhudia burudani hivyo kitendo cha mechi hiyo kutoshuhudiwa mashabiki ni kitendo cha ubakaji wa mpira.
“Huu ni ubakaji wa mpira mfano tuliona timu ya Tabora walipata ajali hiyo sawa,Dodoma Jiji lakini mpaka leo mashabiki hatuelewi kipi kilipelekea mpira wa Yanga na Simba kuhairishwa, nani anajalia maumivu ya hisia zetu na gharama, lazima kanuni zizingatiwe Kila timu ipate haki yake” amesema Hassani.



