Viongozi wapewa mbinu kumaliza kero za wananchi

KATAVI: Mwenyekiti Wa CCM Mkoa wa Katavi, Idd Kimanta amesisitiza utunzaji wa siri za vikao, ushirikiano, upendo, ushirikiano wa chama hicho na viongozi wa Serikali katika kutatua kero za wananchi na kuleta maendeleo.

Kimanta ameyasema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Ilunde Wilaya ya Mlele akiwa katika ziara ya siku sita ambapo amesisitiza ufanyikaji wa vikao na uimarishwaji chama na Jumuiya zake kuelekea kipindi cha Uchaguzi wa Serikali za Vijiji/Vitongoji na Mitaa.

Amewaelekeza viongozi wa matawi, kata na wilaya kushuka kwa wananchi kutatua kero walizonazo sambamba na kuelezea miradi iliyotekelezwa na serikali na inayoendelea kutekelezwa katika maeneo yao.

Advertisement

Katika Kitongoji cha Ibela Mafipa Kijiji cha Ilunde Mwenyeki Kimanta amesikiliza kero mbalimbali za wananchi sambamba na kuwaomba wananchi kuendelea kumuunga mkono Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuleta miradi ya Afya, Elimu na miundombinu katika Mkoa wa Katavi.

Kwa upande wao wakazi wa Wilaya ya Mlele akiwepo Mahona Mashimba amemshukuru Mwenyekiti wa CCM Mkoa katavi kwa kazi anazofanya za kutatua kero za wananchi kwani kufanya hivyo kumeleta tija ya kumaliza baadhi ya migogoro iliyopo ndani ya maeneo yao kama vile migogoro ya ardhi na uhaba wa watumishi.