Vipaumbele 9 Mpango wa Maendeleo wa Taifa vyaelezwa

DODOMA; WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo amewasilisha bungeni Taarifa ya Hali ya Uchumi kwa mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2024/25.

Akiwasilisha bungeni leo Juni 13, 2024, Prof Mkumbo amesema, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2024/25 vimezingatia Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26, Ilani ya CCM kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 na Sera na Mikakati mbalimbali ya kisekta.

Pia amesema mpango umezingatia mipango mingine ya kikanda na kimataifa zikiwemo Dira ya Maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) 2050; Dira ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) 2050; Agenda 2063 ya Maendeleo ya Afrika; na Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030.

Advertisement

“Mheshimiwa Spika, Malengo ya jumla ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2024/2025 ni: “Kuendelea kulinda mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano iliyopita.

“Kuendelea na juhudi za kujitosheleza kwa mahitaji ya chakula nchini kwa kuendelea kuongeza matumizi ya mbolea, mbegu bora na kilimo cha umwagiliaji.

“Kuongeza uzalishaji na uuzaji wa bidhaa (pamoja na huduma) nje ya nchi kupitia sekta za kilimo, ufugaji, uvuvi, misitu na madini.

“Kuweka mkazo wa pekee katika kuongeza thamani katika mazao yanayozalishwa kupitia sekta za kilimo, ufugaji, uvuvi, misitu na madini.

“Kuendelea kuongeza, kuboresha na kuimarisha ubora wa huduma za jamii, ikiwa ni pamoja na elimu, afya, maji na umeme.

“Kuendelea kupanua na kuimarisha miundombinu ya usafiri wa barabara, reli, anga, na majini, na utunzaji endelevu wa mazingira.

“Kujielekeza kwenye kufungua fursa katika sekta za madini ya kimkakati (critical minerals), uvuvi wa bahari kuu (deep sea fishing), uchumi wa kijani (green economy) na uchumi wa kidigitali (digital economy). Maeneo haya matatu, ni maeneo yanayokamata kasi duniani kwa sasa, na ambayo kwa upande wetu hatujavuna ipasavyo.

“Kuendelea kuchukua hatua stahiki katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi, ikiwemo kuetekeleza mkakati wa miaka kumi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.

” Kukamilisha maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,”amesema Waziri Mkumbo.