Vita Sudan changamoto biashara ya mafuta

SUDAN Kusini inakabiliwa na changamoto ya kusafirisha mafuta katika soko la nje baada ya kuibuka vita nchini Sudan na kusitishwa kwa shughuli katika mji mkuu wa Khartoum, ambao unatumika kupitisha bidhaa hiyo.

Msemaji wa Serikali na Waziri wa Habari, Michael Makuei alisema juzi kuwa nchi inakabiliana na kushuka kwa bei ya mafuta, huku wanunuzi wakishusha bei hadi chini ya Dola 70 kwa pipa kutokana na ukosefu wa usalama nchini Sudan.

Kwa mujibu wa Makuei, Waziri wa Mafuta ya Petroli, Puot Kang Chol, aliuambia mkutano wa Baraza la Mawaziri kuwa, ana imani katika ufanyaji biashara wa bidhaa hiyo.

“Alituhakikishia kuwa upatikanaji wa mafuta bado upo licha ya changamoto zilizopo.

“Kuna tahadhari ambazo tayari zimechukuliwa ili endapo kutatokea usumbufu wowote katika upatikanaji wa mafuta, tuwe katika nafasi ya kufanya lolote kukabili hali hiyo,” alisema na kuongeza:

“Kwa sababu ya vita ya Sudan, bei ya mafuta imeshuka kwa sababu kampuni zilizohamisha na kutumia Bandari ya Sudan zinaogopa kupeleka meli zao bandarini Sudan.”

Makuei alisema, serikali inafikiria kutumia kiwanda cha kusafisha mafuta cha Bentiu ambacho bado kinafanya kazi.

Kwa mujibu wa Makuei, Rais Salva Kiir aliamua ubalozi wa Sudan Kusini mjini Khartoum (Sudan) ubaki wazi.

“Hadi sasa, ubalozi wetu uko wazi na unafanya kazi, isipokuwa kwa sehemu ulipigwa na moja ya makombora, hivyo wafanyakazi wa ubalozi watahamishwa tu lakini si kufungwa.”

Habari Zifananazo

Back to top button