Vitabu 2700 kusaidia wanafunzi nchini

SERIKALI ya China imetoa msaada wa vitabu 2700 kwa shule za sekondari Tanzania kwa lengo la kuwezesha ufundishaji na ujifunzaji wa lugha ya Kichina nchini.

Akizungumza wakati wa kupokea vitabu hivyo leo, Mei 26, 2023 jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo amesema ufundishaji wa lugha hiyo kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne hapa nchini umeendelea kuimarika tangu kuanzizshwa kwake mwaka 2016.

Aidha, amesema kwa sasa ziko shule za serikali 18 zinazofundisha lugha ya Kichina, shule mbili ambazo ni Morogoro na Usagara zimechukua hatua zaidi na kufundisha lugha hiyo kwa wanafunzi wa kidato cha tano wanaochukua mchepuo wa Kiswahili, Kingereza na lugha ya Kichina (KEC).

Katibu Mkuu huyo aliongeza na kusema kuwa kwa sasa wizara ipo kwenye mapitio ya sera na mabadiliko ya mitaala na moja ya mapendekezo yaliyopo ni kufundisha lugha mbalimbali ambapo wachina wameanza.

“Nimeelezwa kuwa mwezi Aprili 2023 mligawa vitabu 2,304 na leo vitabu 2,700 na kufanya idadi ya vitabu mlivyotoa kuwa 5004 hii itasidia katika ufundishaji na ujifunzaji wa lugha ya Kichina na kuleta uwiano mzuri wa vitabu kwa wanafunzi,” alisema Profesa Nombo.

Balozi wa China nchini Tanzania, CHEN Mingjian alieleza kufurahihwa na uhusiano baina ya nchi hizo mbili na kusema kuwa anaamini siku zote maarifa yana nguvu, hivyo vitabu vilivyogawiwa vitasaidia walimu na wanafunzi kujifunza lugha ya Kichina kwa ufasaha ikiwa ni pamoja na kuielewa historia ya China na utamaduni wao.

Habari Zifananazo

Back to top button