Vituo 175 vya Watoto mahututi vyaongezwa
SERIKALI imeongeza vituo vyenye vyumba maalumu kwa ajili ya kutoa huduma kwa watoto wachanga wenye umri kati ya sifuri mpaka mitano wenye hali mahututi (Neonatal Care Unit), kutoka 18 mwaka 2017 hadi 175 mwaka 2023.
Hayo yamesemwa Juni na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel Jijini Dodoma.
Amesema, serikali kupitia wizara ya Afya imeweka mipango ya kupunguza vifo vya watoto wenye umri 0 hadi miaka mitano a kwa kuongeza vituo hivyo ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa watoa huduma juu ya namna ya kutoa huduma jumuishi kwa watoto wachanga na watoto ili kuokoa vifo vya watoto hao vinavyoweza kuepukika.
Amesema, Serikali imeendelea kuimarisha huduma za kukinga na kuzuia magonjwa yanayozuilika kwa chanjo kama vile Surua, Nimonia, kuharisha, donda koo, kifaduro, pepo punda na polio kwa kuongeza utoaji wa chanjo za Watoto chini ya Mwaka mmoja kufikia kiwango cha zaidi ya asilimia 98 ya utoaji wa chanjo ya Penta 3.
Aidha, Dkt. Mollel amesema, Serikali imeongeza vituo vinavyotoa huduma kwa watoto waliozaliwa wakiwa na uzito pungufu (Kangaroo Mother Care) ambapo kwa sasa vituo 72 na Hospitali 175 zinatoa huduma hizo
Amesema, mwaka 2023/2024 serikali imepanga kuongeza vituo 100 ili kufikia vituo 275 ifikapo mwezi Juni 2024 vitavyosaidia kuongeza huduma hizo nchini.
Dkt. Mollel amesema serikali imeendelea kuongeza vifaa na vifaa tiba ikiwemo CT-SCAN zimeongezeka kutoka 3 mpaka sasa zipo zaidi ya 50, MRI zilikuwa 2 lakini mpaka sasa zipo zaidi ya 19.