Vituo vya malezi na makuzi fursa kwa wanawake

KAMATI ya Kitaifa ya Ushauri kuhusu utekelezaji wa Programu ya Kizazi chenye Usawa imeridhika na utekelezaji wa Programu hiyo Wilayani Chamwino mkoa wa Dodoma hasa kuwezesha jamii katika malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto ili mama apate muda wa kuendelea na shughuli za kiuchumi.
Nangi Masawe amesema hayo wakati akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo wakati wa siku ya pili ya ziara ya kamati mkoani humo yenye lengo la kufuatilia utekelezaji wa programu hiyo.
Amesema uwepo wa vituo vya malezi na makuzi ni fursa kwa wanawake kuendeleza shughuli zao za kiuchumi kwani wakikosa sehemu sahihi za kuwaacha watoto wao wanaweza kupatwa na madhila ya ukatili na wao pia kukosa fursa mbalimbali za kupata kipato na kufikia usawa wa kijinsia katika uchumi.
Masawe amesema kuwa lengo kubwa la programu ya kizazi chenye usawa siyo tu kumwezesha mwanamke kifedha kupata mtaji wa biashara bali pia kuweka mazingira wezeshi ya kumpunguzia adha katika sekta mbalimbali zikiwemo upatikanaji wa maji, nishati ya umeme, nishati safi ya kupikia na uwezeshaji katika elimu itakayomsaidia kuelekea katika kizazi chenye usawa nchini.
“Jambo mnalofanya hapa walezi wa kituo hiki ni la heri sana na hii ni dhana nzuri katika kuwasaidia watoto wetu katika malezi na pia kutoa fursa kwa wanawake kuendelea na shughuli za kiuchumi ili tuweze kufikia kizazi chenye usawa kama Mheshimiwa Rais alivyoweka ahadi Kimataifa.”amesema Masawe.
Naye Mjumbe wa Kamati hiyo Carolyn Kandusi amesema kuwepo wa vituo vya Malezi sio tu inampunguzia mzazi mzigo wa malezi kwa Mtoto na kukosa muda wa Kufanya shughuli za kiuchumi bali pia inasaidia watoto kupata malezi stahili wakiwa katika vituo husika, hivyo itasaidia kujenga familia, jamii na Taifa lenye uimara katika malezi kwa watoto.
Naye mmoja wa wanufaika wa Kituo cha Malezi na Makuzi ya Awali ya Mtoto katika Shule ya Msingi Chamwino Agness Joram ameishukuru Serikali kwa kuwezesha upatikanaji wa vituo hivyo katika maeneo yao kwani vinawasaidia kupata muda wa kufanya shughuli zao za kiuchumi na kuwapa watoto wao Malezi ya Awali wanayostahili.
/* */