Viwanja 3 kuwaka moto Ligi Kuu leo

Sehemu ya wachezaji wa kikosi cha Simba wakifanya mazoezi.

BURUDANI kwa wapenda soka inaendelea leo kwa michezo 3 ya Ligi Kuu Tanzania Bara kupigwa viwanja tofauti.

Wanamsimbazi, Simba itaikaribisha Coastal Union kwenye uwanja wa KMC uliopo Dar es Salaam.

Simba ipo nafasi ya 3 katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 12 baada ya michezo 4 ikishinda yote wakati Coastal inashika nafasi ya 13 ikiwa na pointi 4 baada ya michezo 6 ikishinda 1, sare 1 na kupoteza 4.

Advertisement

SOMA: Simba watakiwa kutanguliza mbele maslahi ya klabu

Kwenye uwanja wa Lake Tanganyika mjiini Kigoma kutakuwa na patashika nguo kuchanika wakati wenyeji maafande wa Mashujaa itakapomenyana na Singida Black Stars.

Singida Black Stars inaongoza Ligi Kuu ikiwa na pointi 13 baada ya michezo 5 ikishinda 4, sare 1 na haijapoteza wakati Mashujaa ipo nafasi ya 6 ikiwa na pointi 9 baada ya michezo 5 ikishinda 2, sare 3 na haijapoteza mechi.

Huko Mbeya, baada ya kuambulia pointi ya kwanza tangu kukaribishwa Ligi Kuu, Ken Gold itashuka tena dimba la Sokoine kuikabili JKT Tanzania.

JKT Tanzania ipo nafasi ya 10 ikiwa na pointi 7 baada ya michezo 5 ikishinda 1, sare 4 na haijapoteza wakati Ken Gold ni ya mwisho wa msimamo wa ligi ikicheza mechi 6, sare 1 na kupoteza 5.