Vodacom yatoa fursa wawekezaji wadogo

DAR ES SALAAM: KAMPUNI ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania imeongeza kasi ya uwekezaji katika ubunifu wa kidijiti kwa ajili ya kuwawezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs), katika hatua inayolenga kuchochea ukuaji jumuishi na kuimarisha muhimili wa uchumi wa taifa.

Kupitia mipango bunifu ya kidijiti kampuni hiyo inalenga kubadili namna wafanyabiashara hao wanavyoendesha biashara kwa kuwapa teknolojia nafuu na ya kuaminika inayoongeza ufanisi wa kazi, kuboresha huduma kwa wateja na kujenga msingi imara wa ukuaji wa muda mrefu.

Mkurugenzi wa Biashara wa Vodacom Tanzania, Nguvu Kamando, alisema hayo Dar es salaam katika mjadala wa mtandaoni uliolenga kuchambua fursa na maarifa ya vitendo.

Akizungumza hayo alibainisha kuwa wafanyabishara hao ni muhimili muhimu kwa uchumi wa taifa, hivyo hatua hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa kampuni wa kuharakisha ujumuishwaji wa kidijiti.

“Uzoefu kutoka katika nchi zilizoendelea unaonesha kuwa mageuzi endelevu ya kiuchumi hupatikana kwa kuwawezesha kwa makusudi wafanyabiashara wadogo na wa kati, ambao ni injini ya maendeleo katika jamii zao,” alisema Kamando.

Aliongeza bishara ndogo na za kati zinachangia zaidi ya asilimia 95 ya biashara zote, takribani asilimia 35 ya Pato la Taifa (GDP), na kuajiri zaidi ya watu milioni tano wengi wao wakiwa katika sekta za kilimo na huduma.

Alisema pamoja na mchango wao katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini, biashara hizi ndogo hasa za kiwango cha chini na changamoto kadhaa ikiwemo ukosefu wa mitaji, viwango vya juu vya riba, mazingira magumu ya udhibiti na miundombinu isiyotosheleza.

Kamando alisema upatikanaji mdogo wa miundombinu nafuu ya Teknolojia ya Habari (TEHAMA) ni miongoni mwa changamoto kubwa kwa biashara ndogo, huku nyingi zikilazimika kutumia gharama kubwa kuajiri wataalamu wa Tehama au kuwekeza katika seva na vituo vya kuhifadhi data.

Alisema Vodacom imeanzisha huduma za kidijiti zinazohifadhiwa mtandaoni , ambazo zinaondoa hitaji la kununua vifaa vya gharama kubwa au kuanzisha vituo vya data ndani ya kampuni, lengo ni kukabili changamoto hizo.

Alisema huduma hizo zinawawezesha wafanyabishara hao kupata miundombinu salama na ya kuaminika kwa gharama nafuu zaidi, na hivyo kuwapa nafasi ya kuelekeza nguvu zao katika kukuza biashara na ubunifu.

Kamando alibainisha kuwa sehemu kubwa ya miamala nchini bado inafanyika kwa fedha taslimu, akisisitiza umuhimu wa kuharakisha matumizi ya malipo ya kidijiti ili kuongeza ufanisi, uwazi na tija ya jumla ya uchumi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button