DODOMA: SERIKALI imevitaka vyuo vyote nchini kujiendesha kibiashara badala ya kutegemea ruzuku ya fedha za matumizi yao kutoka Serikali Kuu.
Akihutubia katika mahafali ya 15 ya Chuo cha Serikali ya Mtaa Hombolo nje kidogo ya Jiji la Dodoma Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI (ELIMU), Deogratius Ndejembi ambaye alimwakilisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amevitaka vyuo vyote nchini kujiendesha kibiashara kwa kubuni vyanzo vya mapato ikiwa ni pamoja na kuwatumia watafiti wabobezi kufanya tafiti.
“Chuo hiki kinayo hazina ya wabobezi wa fani mbalimbali fanyeni utafiti na kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kupunguza utegemezi, vilevile endeleeni kutenga fedha kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya kuendeleza miradi ya maendeleo na shughuli nyingine zinazohusu ustawi wa chuo” amesema Ndejembi.
Ndejembi pia amesema azma ya Rais, Samia Suluhu Hassan ambaye alifanya kikao na Watendaji wa Taasisi mbalimbali nchini Agosti, 2023 ni kuona mashirika ya Umma yanaongeza tija katika uzalishaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi na kupunguza utegemezi wa ruzuku kutoka mfuko wa serikali Kuu.
“nasisitiza mashirika na Taasisi za Serikali ziendelee kubuni mikakati ya kuongeza mapato ili faida itumike kuendesha shughuli za taasisi na kutoa gawio serikalini, maelekezo haya yanahusu pia jumuiya ya chuo hiki, ongezeni kasi ya kuibua mikakati inayotekelezeka na yenye tija” amesema Ndejembi.
Ndejembi akijibu kuhusu kero ya kuwekwa lami barabara ya Ihumwa hadi Hombolo alisema tayari upembuzi yakinifu umefanyika lakini ameuagiza Wakala wa Barabara nchini (TANROAD) kufuatilia kwa karibu suala hilo ili kazi ianze kwa wakati baada ya kukamilika taratibu zote.
Akisoma risala kabla ya hotuba ya mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo (LGTI), Profesa Joseph Kusilwa ametoa ombi la kupatiwa fedha kwa ajili ya ujenzi wa majengo pacha ya kampasi ndani ya jiji la Dodoma baada ya kupata eneo la ilipokuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ili kuondokana na adha ya kulipa kodi inayofikia shilingi milioni 75 kwa mwaka kwani upembuzi yakinifu umekwishafanyika lakini ufinyu wa bajeti ni kikwazo kwao.
Kwa upande wake akitoa maelezo ya awali, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo (LGTI) Dk Mashala Yusuph amesema chuo hicho kimepewa jukumu la kuzijengea uwezo Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini kwa kutoa mafunzo ya muda mrefu na mfupi, kufanya tafiti na kutoa ushauri elekezi ambapo mpaka sasa fani sita zinatolewa kwa kuzingatia mahitaji ya wateja ambao ni Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Naye Mkuu wa chuo hicho Dk Danford Sanga amesema jumla ya wahitimu 4,666 wamehitimu katika mahafali hayo ya 15 tangu chuo hicho kianze kutoa mafunzo ya muda mrefu mwaka 2007 kwa ngazi za astashahada ya awali, stashahada na shahada ya kwanza na kwamba matarajio yao ni kuona wahitimu hao wanatoa huduma bora kwa jamii zinazowazunguka.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya wanafunzi Stephen Thomas ametoa ombi la kupatiwa mikopo kama ilivyo kwa vyuo vingine vya kati ili waweze kujikimu katika masomo yao, pia kupatiwa kipaumbele kwenye ajira za Serikali na kuwekwa lami kwa barabara ya Ihumwa hadi Hombolo ili kuondoa adha ya usafiri na kukipa chuo hicho hadhi.