‘Waacheni viziwi watumie fursa zinazowazunguka’

MBEYA; WAUMINI wa dini ya Mashahidi wa Yehova wameiasa jamii wasiwafiche nyumbani viziwi na badala yake kuwawezesha kunufaika na fursa zinazowazunguka kwenye maeneo yao, ili kutowafanya wanyonge na wenye kujiona wanatengwa.

Miongoni mwa fursa wanazopaswa kunufaika nazo ni pamoja na za mafundisho ya kidini, yenye kuwawezesha kuishi kwa kumtumikia Mwenyezi Mungu na kuishi maisha yenye amani na upendo kwa kushirikiana kwa karibu na wana jamii wengine.

Hayo yamebainisha kwenye kambi maalumu ya utoaji mafundisho ya biblia kwa viziwi inayoendelea katika Viwanja vya Ruandanzovwe jijini Mbeya, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Viziwi Duniani itakayofanyika kitaifa mkoani Mbeya keshokutwa.

Advertisement

Msemaji wa dini ya Mashahidi wa Yehova Mkoa wa Mbeya, Jovenary Joseph  amesema katika kushiriki Wiki ya Viziwi duniani wanatarajia kufikisha mafundisho ya Biblia kwa zaidi ya viziwi 500 wanaotarajiwa kuja mkoani Mbeya kushiriki kilele cha wiki hiyo.

Amesema kwa kutambua Mungu wanayemtumikia Mashahidi wa Yehova hana ubaguzi,  kwa kuwa anawajali watu wake wa namna zot,e wameamua kujikita kwenye utoaji elimu ya Biblia kwa njia ya ishara kwa viziwi wakitambua kuwa kundi hilo pia linalo uhitaji mkubwa wa kuyajua mafundisho yake.

“Viziwa pia wanao uhitaji wa kufikiwa na habari za Ufalme wa Mungu au neno lake kwa ujumla.

Wakijifunza neno la Mungu kupitia lugha yao inaweza kuwa rahisi kuifikia mioyo yao na wanaweza kuhisi kuwa pamoja na Mungu,” amesema Joseph.

Elisha Mwakapombe ambaye pia ni mtafsiri wa lugha ya ishara kati ya wafundishaji na viziwi amesema wanatoa huduma ya mafundisho ya elimu ya biblia kwa kundi hilo bila malipo, ili kuliwezesha kuwa na ustawi wa kiroho sawa na wana jamii wengine.

1 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *