Waamuzi Tanzania wafuatilie, wajifunze kwa wenzao CHAN

MICHUANO ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN 2024) inatarajiwa kuanza Agosti 2, mwaka huu.

Mataifa ya Afrika Mashariki; Tanzania, Kenya na Uganda kwa mara ya kwanza yanaandaa michuano hiyo kwa pamoja.

Ni michuano inayofanyika kwenye ardhi ya nyumbani huku tukiheshimiwa kwa kupewa sherehe za ufunguzi zitakazofanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ambapo Taifa Stars itaikabili Burkina Faso.

Sherehe za fainali zitafanyika Kenya Agosti 30 na ya mshindi wa tatu zitakuwa Uganda.

Kuna namna mbalimbali mtu anaweza kuamua kutazama mashindano haya, mwingine akaamua kuangalia namna gani Taifa Stars itafanya vizuri uwanjani kitu ambacho kila Mtanzania anatamani.

Mwingine anaweza kuamua kuangalia upande wa kutumia fursa za kiuchumi zitakazoambatana na michuano hii kuandaliwa nyumbani, kila mmoja na upande utakaomvutia.

Upande wetu pamoja na kuwa na maeneo mazuri mengi ambayo tungeweza kuyaangazia au tutakuja kuyatupia macho kwa siku za usoni, leo tungependa kuangalia upande wa waamuzi.

Waamuzi bora wa bara la Afrika ndio ambao wamepewa nafasi ya kuchezesha kwenye michuano hii na hata Tanzania pia tumewatoa wakina Ahmed Arajiga na Hamdani Said.

Tungependa kuwapongeza waamuzi hawa kwa maana ubora wao umeweza kuonekana na Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), kiasi cha kupewa dhamana hii.

Lakini kutoa waamuzi wawili katika kundi la waamuzi wengi kwenye soka letu, tafsiri yake ni kwamba Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia kamati yake ya waamuzi inayoongozwa na Mwenyekiti wake Nassoro Hamduni ina kazi ya ziada ya kuhakikisha inatengeneza waamuzi wengi zaidi ambao wote tutajivunia kama taifa.

Tafsiri ni nyingine ni kwamba malalamiko ya wadau kwa miaka kadhaa sasa na zaidi msimu uliomalizika hasa wa Ligi Kuu Tanzania Bara juu ya uwezo mdogo wa waamuzi wetu yamepata mashiko baada ya kuona tumetoa waamuzi watatu kati ya wengi.

Hapa tunataka kusema waamuzi wetu wote na wa madaraja yote wana uwezo mkubwa wa kuwa miongoni kati ya walio bora sio tu Afrika, bali na duniani kwa ujumla kama wataamua kwa dhati ya mioyo yao kujifunza kutoka kwa walio bora na kwa kuanzia wafanye hivyo kwenye michuano hii ya Chan.

Wakati tunaiombea Taifa Stars ifanye vizuri kwenye michuano hii pia tunawaombea waamuzi wetu wachezeshe vizuri mechi watakazopangiwa lakini pia tunawaomba wale ambao hawajapata nafasi za kuchezesha kwenye mashindano haya basi wajifunze kwa walio bora ili nao wawe bora siku zaidi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button