VIONGOZi wa Klabu za waandishi wa habari kwenye mikoa mbalimbali nchini, wamesisitizwa kusimamia na kutetea maslahi yanayohusu waandishi wa habari wenyewe badala ya kusubiri watu wa nje kuwasemea.
Akifungua leo mafunzo ya siku tatu ambayo yameandaliwa na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), ,koani Morogoro, Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha, Claud Gwandu amesema ni wakati sasa viongozi wa vyama vya habari nchini kuhakikisha wanasimamia vyema maslahi na changamoto za wanahabari kupitia vyama vyao.
Amesisitiza lazima vyama visimamie vyema matumizi ya fedha za vyama, kutatua changamoto kwa wanahabari ikiwemo usimamizi wa maadili kwa wanahabari, ili heshima na taaluma ya uandishi izingatiwe.
Ameipongeza UTPC kwa kutoa mafunzo kwa viongozi wa vyama vya wanahabari mikoa ya Manyara, Arusha, Tanga na Kilimanjaro na kanda nyinginezo katika kuhakikisha masuala ya uongozi na fedha yanasimamiwa vyema na viongozi wa klabu, ili kufikia malengo ya klabu.