Waandishi watakiwa kutoa elimu ya PPRA Mtwara

WAANDISHI wa habari mkoani Mtwara wametakiwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia Mfumo wa Usimamizi wa Ununuzi wa Umma (PPRA) ili kudhibiti ubora wa miradi ya serikali.

Akizungumza mkoani Mtwara wakati wa mafunzo ya siku moja kwa waandishi, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Abdallah Mwaipaya amesema wafanyabiashara wafanye kazi na serikali kupitia mfumo huo wa ununuzi.

Mafunzo hayo ni kuhusu kuwajengea uwelewa zaidi wanahabari hao juu ya suala zima la mfumo wa usimamizi wa ununuzi wa umma yaliyoambatana na uzinduzi wa ofisi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma Kanda ya kusini hafla iliyofanyika katika Manispaa ya Mtwara Mikindani.

Aidha wilaya hiyo ni moja kati ya wilaya za Kanda ya kusini ambazo zina fursa nyingi za kiuchumi za sekta mbalimbali na wananchi wenye nguvu na nia ya kuchangia kwenye maendeleo ya taifa.

“Hapa Mtwara na maeneo mengine mengi ya kusini kuna wafanyabiashara wengi lakini tunafahamu baadhi yao hawafahamu jinsi gani wanaweza kufanya biashara na serikali”amesema Mwaipaya

Ameongeza kuwa, Sasa ni jukumu letu sisi kuweza kuwafahamisha kwamba kuna PPRA wao wanayo nafasi kubwa ya kuweza kuwaelekeza namna gani wafanyabiashara wetu wanaweza kufanya kazi na serikali”

Meneja wa PPRA Kanda ya kusini, Fenias Manasse ameyataja baadhi ya majukumu ya kitengo cha ununuzi ikiwemo kutambua ubora wa bidhaa, kuhakikisha taasisi zinazingatia sheria na zingine.

Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari mkoani humo, Grace Kasembe kwa niaba ya waandishi ameishukuru PPRA kwa kuwapatia elimu hiyo na kuahidi kuwa mabalozi wazuri wa kuhabarisha umma kuhusu elimu hiyo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button