Wabainika kutanuka moyo baada ya uchunguzi

NUSU ya watu 335 waliopata huduma ya uchunguzi na matibabu ya moyo katika kambi maalum iliyofanyika kwa siku mbili mwishoni mwa wiki katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group wamebainika kuwa na matatizo ya shinikizo la damu na matatizo ya kutanuka kwa moyo, mishipa ya damu na matatizo ya kutanuka kwa moyo, mishipa ya damu ya moyo kuziba.

Matatizo mengine yaliyobainila ni pamoja na mafuta mengi kwenye mishipa ya damu, maumivu ya kifua, shida za valvu, shida ya mfumo wa umemewa moyo pia tumewaona watoto waliokuwa na matatizo ya matundukwenye moyo na mishipa ya damu ya moyo kutokukaa kwenye mpangilio wake”

Kaimu Mkurugenzi wa hospitali hiyo Dk.Tulizo Shemu amesema matibabu hayo ya tiba mkoba yajulikanayo kwa jina la Rais Dk Samia Suluhu Hassan yalifanyika maalumu kwa ajili ya kusogeza huduma za kibingwa za matibabu ya moyo kwa wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam na mikoa ya jirani.

Dk Shemu ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo amesema katika kambi hiyo watu waliowaona walitoka ndani na nje ya mkoa wa Dar es Salaam na wengi wao walikuwa na tatizo la shinikizo la juu la damu pamoja na matatizo mengine ya moyo.

“Nusu ya watu tuliowaona walikuwa na tatizo la shinikizo la juu la damu na wengine walikuwa na matatizo ya kutanuka kwa moyo, mishipa ya damu ya moyo kuziba, mafuta mengi kwenye mishipa ya damu, maumivu ya kifua, shida za valvu, shida ya mfumo wa umeme wa moyo,” alisema na kuongeza kuwa pia waliwahudumia watoto waliokuwa na matatizo ya matundu kwenye moyo na mishipa ya damu ya moyo kutokukaa kwenye mpangilio wake.

“Tuliowakuta na shida za moyo na wengine waliokuwa na shida mbalimbali za mwili kama vile masikio, mifupa, ngozi, macho tumewapeleka katika kliniki zetu kwaajili ya matibabu kwani katika hospitali hii licha ya kutibu moyo tunatibu pia magonjwa mengine pia wengine tumewapa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)”, amesema Dk Shemu.

Dk Shemu amesema kambi za aina hiyo zitakuwa zinafanyika mara kwa mara katika Hospitali hiyo kwani kwa kufanya hivyo wananchi wengi wa mkoa wa Dar es Salaam na mikoa jirani watafikiwa na huduma za kibingwa za matibabu ya moyo.

Kwa upande wao wananchi waliopata matibabu katika kambi hiyo wameishukuru Serikali kwa huduma waliyoipata na kuomba iwe endelevu ili watu wengi zaidi waweze kufikiwa na huduma za kibingwa za matibabu ya moyo.

Tatu Hassan mkazi wa Shinganya amesema aliona tangazo kwenye televisheni la kufanyika kwa matibabu hayo na kuchukuwa hatua ya kwenda kufanyiwa uchunguzi na matibabu ya moyo.

“Ninaishukuru Serikali kwa kutuangalia wananchi wanyonge wenye kipato cha chini na kutufikishia huduma hii ya matibabu ya kibingwa. Nimefika hapa nimefanyiwa vipimo, nimepewa ushauri na dawa za kwenda kutumia mwezi mmoja kwani mimi ninatatizo la shinikizo la juu la damu ambalo limepelekea moyo wangu kutanuka”, alisema Tatu.

“Ninatoa wito kwa wananchi wenzangu wanapoona matangazo ya upimaji wa magonjwa mbalimbali wasipuuze wawahi hospitali mapema kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na kupata matibabu mapema kuliko kusubiri hadi waumwe ndipo waende kutibiwa”, ameseema Richard John mkazi wa Tegeta.

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imekuwa ikitoa huduma ya tiba mkoba ya kuwafuata wananchi mahali walipo kwa kufanya uchunguzi na matibabu ya moyo katika maeneo mbalimbali hapa nchini. Hadi sasa wameshatoa huduma hiyo katika mikoa 12 na kuona watu 7196 ambapo 847 walikutwa na matatizo ya moyo yaliyohitaji matibabu ya kibingwa na kupewa rufaa ya kwenda kutibiwa.

Habari Zifananazo

5 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button