Wabunge EALA pelekeni mnachotumwa

WIKI iliyopita, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, liliwachagua wagombea tisa kuwakilisha Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA).

Miongoni mwa waliochaguliwa, wanane wanatoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mmoja yaani Mashaka Ngole akitoka katika chama cha upinzani cha CUF (Chama cha Wananchi).

Waliochaguliwa kutoka CCM ni Angela Kizigha, Nadra Mohamed, Dk Shogo Mlozi, Dk Abdulla Hasnuu Makame, Machano Ali Machano, Ansar Kachwamba, James Millya na Dk Ng’waru Maghembe.

Tunawapongeza wabunge waliochaguliwa ili wakajiunge na wenzao kutoka nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambayo ndio yenye bunge hili, EALA.

Ikumbukwe kuwa, nchi nyingine wanachama wa EAC ni Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na mwanachama mpya yaani, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Bunge linalomaliza muda wake yaani Bunge la Nne lina wajumbe 62 ambao ni wabunge tisa kutoka kila nchi mwanachama isipokuwa DRC iliyojiunga hivi karibuni.

Kama ilivyojili katika uchaguzi huu wa wabunge wa EALA, wabunge hao, huchaguliwa na bunge la nchi husika kuwakilisha taifa zima.

Wabunge wengine wanane (katika Bunge la Nne) walitokana na nyadhifa zao.

Kwa lugha nyingine tunasema, nchi wanayotoka wabunge husika, ndiyo ‘jimbo lao la uchaguzi’ hivyo, wana kazi kubwa ya kuhakikisha wanatetea na kupigania kwa nguvu zote maslahi ya jimbo (nchi) lao kabla ya kitu kingine chochote katika EALA.

Ni kwa msingi huo tunapowapongeza kwa kuchaguliwa kwao huku pia tukiwapongeza wanaomaliza muda wao katika chombo hicho cha EAC, tunapenda kuwakumbusha wabunge wateule kuwa, wamechaguliwa ili kubeba na kulinda agenda za Watanzania kama wabunge wa nchi nyingine wanavyobeba na kulinda agenda na maslahi ya nchi zao.

Tunasema, katu hatutarajii kuona wala kusikia kuwa, baada ya kuchaguliwa na kuapishwa, wabunge wa EALA badala ya kuwakilisha nchi yao na watu wake, sasa wanabadilika na kujiwakilisha wao na familia zao.

Tunasema hivyo tukiwakumbusha kuwa, hata inapotokea kuna mgongano wa kimaslahi au mgongano wa kimawazo kati ya nchi yao na upande au ngazi nyingine, wakumbuke kuwa wametumwa na Watanzania kuwakilisha mawazo, matakwa na maslahi ya Watanzania na si vinginevyo.

Wabunge wetu wa EALA waende bungeni na agenda za Watanzania kutoka kwa Watanzania si agenda kuhusu Watanzania kutoka katika familia, nyumbani au mifukoni kwao.

Kutembea na agenda za Watanzania kutoka kwa Watanzania kutakuwa na maana kwao kama wawakilishi wa watu tofauti na baadhi ya wabunge nchini ambao wamekuwa hawaendi katika majimbo yao wala kujua changamoto zilizopo matokeo yake, wanakwenda bungeni tu, kusubiri posho na marupurupu yaliyopo jambao ambalo si jema.

Ndio maana tunasema, wabunge EALA wapeleke wanachotumwa na Watanzania wasiende kuwa wabunge wa “ndio mzee” ili kujinufaisha kwa gharama ya Watanzania.

 

 

 

 

         

Habari Zifananazo

Back to top button