Wabunge, madiwani wapewa hati pongezi

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Iringa kimetoa hati za pongezi kwa wabunge na madiwani wanaotoka Halmashauri ya Wilaya hiyo kutokana na mchango wao mkubwa katika kutekeleza Ilani yao ya uchaguzi.

Hati hizo zimetolewa leo na Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo Constatino Kiwele katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM ya Wilaya ya Iringa iliyokuwa inapokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2022 hadi 2023.

Hati hizo zimetolewa kwa madiwani 38 ambao kati yao 10 ni wa viti maalumu pamoja na Mbunge wa Jimbo la Isimani William Lukuvi na Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Jackson Kiswaga.

Akikabidhi hati hizo zilizotolewa pia kwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Salim Asas na mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, Festo Kiswaga mwenyekiti huyo alisema:

“Kwa kasi hii ya utekelezaji wa Ilani hatuna cha kumlipa Rais Dk Samia Suluhu Hassan zaidi ya kumuahidi ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa serikali za mitaa unatarajiwa kufanyika mwakani.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani katika kipindi hicho, Mkuu wa Wilya ya Iringa Veronica Kessy alisema kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, halmashauri ya wilaya hiyo ina jumla ya watu 315,354 ambao kati yao wanawake ni 161,798.

Katika kutekeleza Ilani hiyo, Kessy alizungumzia hali ya watumishi na stahiki zao mbalimbali za utumishi na ajira za watumishi wapya akisema katika kipindi hicho halmashauri hiyo ilipata kibali cha nafasi za ajira mpya 175 katika kada ya elimu, afya na watendaji wa vijiji.

Alitaja maeneo mengine yaliyotekelezwa kuwa ni pamoja na ukusanyaji wa mapato ya ndani akisema hadi Juni 2023 zaidi ya Sh Bilioni 3.9 sawa na asilimia 99 ya makadirio ya mwaka yalikusanywa.

Katika kutekeleza Ilani hiyo, Kessy alizungumzia pia utekelezaji wa miradi mbalimbali, mapambano ya umasikini na uwezeshaji wananchi kiuchumi, kilimo, utalii na masuala mbalimbali yanayohusu ardhi.

Mengine ni pamoja na maendeleo ya huduma ya elimu, afya, maji, barabara, nishati ya umeme, uboreshaji wa kazi za mamlaka za serikali za mitaa na hali ya ulinzi na usalama.

Habari Zifananazo

Back to top button