Wabunge wapitisha bajeti Wizara ya Ardhi
DODOMA; WABUNGE leo Juni 27, 2024, wamepitisha makadirio ya mapato na matumizi kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Ijumaa Mei 24, 2024, Waziri wa Ardhi, Nyumba ya Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa aliwasilisha hotuba yake na kuliomba Bunge lijadili na kuidhinisha kiasi cha Sh Bilioni 169, ili wizara hiyo iweze kutekeleza vipaumbele mbalimbali.
Baadhi ya vipaumbele hivyo ni kuongeza kasi ya upangaji, upimaji na umilikishaji wa ardhi mijini na vijijini, kuimarisha mifumo ya utatuzi wa migogoro ya ardhi na kuimarisha mifumo ya TEHAMA katika utunzaji wa kumbukumbu, utoaji wa huduma na upatikanaji wa taarifa za ardhi.
Vipaumbele vingine ni kuhakikisha uwepo wa nyumba bora, ukuaji wa sekta ya milki na maendeleo ya makazi kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii na kuimarisha mipaka ya kimataifa.
Wabunge mbalimbali wamechangia hotuba hiyo tangu Ijumaa hadi leo jioni Waziri Silaa alipofanya majumuisho ya hoja mbalimba za wabunge na kisha wabunge kupitisha bajeti hiyo.
Isome pia:https://habarileo.co.tz/waziri-silaa-aja-na-vipaumbele-5-ardhi/
Wakati akiwasilisha hotuba yake ya makadiri ya mapato na matumizi, Waziri Silaa amesema miongoni mwa majukumu ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambayo yatafanikisha vipaumbele vya wizara hiyo ni kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi, kusimamia upangaji wa miji na vijiji, kupima ardhi na kutayarisha ramani, kutoa hati za kumiliki ardhi na hatimiliki za kimila, kusajili hati za umiliki ardhi na nyaraka za kisheria pamoja na kuthamini mali.
Majukumu mengine ni kuhamasisha na kuwezesha wananchi kuwa na nyumba bora, kutatua migogoro ya ardhi na nyumba, kusimamia upatikanaji na utunzaji wa kumbukumbu za ardhi, kusimamia ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali yatokanayo na huduma za sekta ya ardhi.
Isome pia:https://habarileo.co.tz/waziri-silaa-angata-mapapa-wa-ardhi/
Kusimamia Shirika la Nyumba la Taifa, Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba na Vifaa vya Ujenzi na Wakala wa Uendelezaji wa Mji Mpya wa Kigamboni, kusimamia uendeshaji wa vyuo vya ardhi vya Tabora na Morogoro na kusimamia maslahi na utendaji kazi wa watumishi wa sekta ya ardhi.