Wabunge, wasomi waipa ‘tano’ serikali kufuta tozo

SERIKALI imepongezwa kwa kusikiliza kilio cha wananchi na kupunguza baadhi ya tozo za miamala ya kielektroniki kuanzia Oktoba Mosi, mwaka huu.

Pongezi hizo zilitolewa na wabunge na wachumi jana walipozungumza na gazeti hili kuhusu maoni yao baada ya hatua ya serikali iliyotangazwa bungeni Dodoma jana na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba.

Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia Dar es Salaam, Abbas Mwalimu alisema kitendo cha kupunguza tozo hizo ni hatua nzuri kwa sababu kwenye utawala bora pamoja na kuwepo vipengele vingi, kimojawapo ni serikali inapaswa kuwa sikivu kwa wananchi wake.

“Kitendo cha kupunguza tozo hizi za miamala ya simu kwa asilimia 10 hadi 50 tayari kinaonesha serikali ni sikivu kwa wananchi wake. Sasa jambo la msingi ni kuongeza wigo wa walipakodi na kuweka uwazi wa matumizi ya fedha zinazotokana na tozo hizi,” alisema Mwalimu.

Alisema wakati Dk Mwigulu akizungumzia punguzo la tozo hizo bungeni, alibainisha wazi kuwa zilikuwa zinatumika katika miradi mbalimbali kama vile kujengea madarasa, mikopo ya elimu ya juu, ujenzi wa zahanati, barabara na hata kuchangia ajira.

“Hili ndio la msingi zaidi kwa sababu watu wanataka kujua thamani ya fedha zao. Imepatikana kiasi gani na imetumika kwenye nini. Ni vyema ukawekwa utaratibu kila mwezi hata kupitia wakuu wa wilaya kutangaza namna fedha hizi za tozo zinavyotumika kwenye miradi ya maendeleo,” alishauri Mwalimu.

Aidha, alishauri kuangalia zaidi sekta zisizo rasmi na kuzirasimisha, akitolea mfano sekta ya usafirishaji kuwa kwa jinsi ilivyo inapaswa kurasimishwa na kuchangia katika kodi.

“Unakuta mtu ana mabasi 20, ana watu zaidi ya 20, lakini hawajaajiriwa wote hawa hawalipi kodi,” aliongeza.

Pia, alishauri kuhusu kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha za serikali ili zitumike kwenye miradi inayostahili pamoja na kuongezea ufanisi maeneo ya kimkakati kama vile bandari yazalishe zaidi na kuongeza pato la nchi.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mchambuzi wa masuala ya uchumi, Profesa Humphrey Mushi alisema punguzo la tozo limeonesha serikali ni sikivu, lakini pia limetoa somo juu ya umuhimu wa kufanyika ushirikishwaji wa makundi mbalimbali wakiwamo wataalamu kinapoanzishwa kitu kipya.

Aidha, alishauri zitafutwe mbinu mbadala zitakazosaidia kupatikana kwa fedha za utekelezaji wa miradi inayotokana na tozo hizo zilizopunguzwa zikishirikisha pia wakwepa kodi.

“Maendeleo yakipatikana yanatumiwa na wote wakiwemo wakwepa kodi. Zikitengenezwa barabara au zahanati wakwepa kodi pia wanazitumia…zitafutwe mbinu nao wabanwe walipe kodi kwa faida ya wote,” alisema Profesa Mushi.

Mbunge wa Mwanga, Joseph Tadayo (CCM) alielezea chimbuko la kuanzishwa kwa tozo hizo kuwa ni kutekeleza miradi muhimu inayogusa zaidi wananchi na kwamba pamoja na umuhimu huo, kutokana na hali ya maisha kuzidi kuwa ngumu serikali imeamua kuwapunguzia mzigo wananchi.

Hata hivyo, alisema kuna umuhimu wa serikali kuangalia uwekezano wa kuongeza wigo wa walipa kodi hali itakayosaidia kutekeleza kwa ufanisi miradi muhimu kutokana na ukweli kuwa wanaolipa kodi kwa sasa hawafiki watu milioni tano.

“Kilichonifurahisha ni serikali kuwasikiliza wananchi wake kwa kupunguza tozo, lakini miradi iliyopangwa kutekelezwa kwa fedha hizo haitasitishwa bali itaendelea.

“Nawaomba wananchi hasa wananchi wangu wa Mwanga wasiwe na wasiwasi kuhusu miradi inayotekelezwa jimboni kwangu,” alisisitiza.

Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa (CCM) alisema pamoja na serikali kufuta na kupunguza baadhi ya tozo, tozo hizo kwa kipindi kifupi zimefanya mambo makubwa kama ujenzi wa zahanati, vituo vya afya, barabara za vijijini ikiwamo pia miradi ya maji.

“Ukweli ni kwamba serikali ilikuwa na nia njema kupitia fedha hizi, ilikuwa inatenga shilingi bilioni 100 kila mwezi kama ruzuku ya mafuta na ilitenga shilingi bilioni 150 za ruzuku ya mbolea na kila jimbo tuligawiwa fedha kujenga madarasa na zahanati,” alisema Vita.

Mbunge wa Momba, Condester Sichalwe (CCM) aliipongeza Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuchukua hatua hiyo na kusisitiza kuwa imeonesha mfano kwani hakuna serikali inayoweza kuendelea kuongoza kwa amani ikiwa wananchi wake wanalalamika.

“Serikali ilikuwa na nia njema na tozo hizi lakini sasa kipindi hiki kuna matatizo kama vile Covid-19 na upungufu wa mvua hivyo ilikuwa ni lazima wananchi wapewe comfortability,” alisisitiza Sichalwe.

 

 

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x