DODOMA: Wachambuzi wa mifumo ya TEHAMA (Business Analysts) katika taasisi za umma wameshauriwa kujiimarisha kielimu ili kuendana na kazi ya ukuaji wa tekonolojia ikiwamo ujuzi katika uchambuzi wa takwimu na akili bandia.
Ushauri huo umetolewa na Kaimu Meneja wa Ushauri na Uelekezi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Joan Valentine wakati akifungua mafunzo ya siku sita kwa wachambuzi wa mifumo ya TEHAMA kwa wataalamu kutoka taasisi za umma.
Alisema ni vyema maafisa hao kujiimarisha na kujifunza kujifunza stadi mbalimbali ikiwemo teknolojia ya akili bandia na uchambuzi wa takwimu, ili ziwasaidie kupambana na mabadiliko ya teknolojia yanayoibuka kwa kasi.
Alisema hatua hiyo itasaidia kuhakikisha ukuaji wa teknolojia hizo unawezesha ukuaji wa taasisi zao.
“Kwa sasa dunia inazungumza kuhusu akili bandia, hivyo wachambuzi wa mifumo lazima muwe na ujuzi wa hizi teknolojia ili kuzisaidia taasisi zenu katika utendaji kazi wa kila siku.
”
Kwa upande wa Mratibu wa Mafunzo hayo, Ceaser Mwambani ambaye pia ni mchambuzi wa mifumo ya TEHAMA, alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo maofisa hao katika maeneo ya uchambuzi wa mifumo ya TEHAMA, usimamizi wa miradi ya TEHAMA, miongozo, viwango, usimamizi, ubora na usalama wa mifumo ya TEHAMA serikalini.