Wachimbaji Geita watakiwa kuzingatia mazingira

BARAZA la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limewataka wachimbaji wadogo na wa kati mkoani Geita, kuhakikisha wanazingatia kanuni za mazingira, ili uwekezaji wao usiwe kikwazo kwa afya zao na Watanzania wengine.
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Samuel Gwamaka, amesema hayo, wakati akizungumuza na waandishi wa habari, baada ya Bodi ya Wakurugenzi NEMC kuhitimisha ziara katika migodi midogo, ya kati na mikubwa mkoani Geita.
Amesema NEMC inatamani kuona uchimbaji mdogo na wa kati unafanyika kwa tija katika miundombinu rafiki na kufuata miongozo ya leseni, ili shughuli hizo ziwe kiwanda cha ajira na siyo chanzo cha magonjwa na ulemavu.
“Kwa hiyo nafikiri sisi kama NEMC, kama bodi tutashirikiana na tume ya madini, pamoja na Stamico kuona kwa kiasi gani ambavyo mazingira ya wachimbaji wadogo maeneo yote wanapofanyia kazi basi palingane na wenzetu wale wa nje.
“Waendeshe uchimbaji kitaalamu, wafuate taratibu za mazingira, wafuate taratibu za kistaarabu za uanzishwaji wa migodi, utafiti wa migodi, uchenjuaji wa madini, na hatimaye na wao waweke mazingira yetu katika hali ya usalama,” amesema.
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya NEMC, Said Tunda amesema lengo la ziara yao siyo kufungia migodi, bali ni kukagua, kutathimini na kushauri njia sahihi ya kuendesha shughuli za uchimbaji wa madini, ili kulinda afya na mazingira.
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Kati wa Kampuni ya Busolwa Mining, Bart Mkinga amekiri kupokea malekezo ya Nemc na kuyafanyia kazi, ili kuendeleza uwekezaji wao mbali na kuchangia pato la taifa pia uwe na tija katika mazingira.
Meneja wa Mgodi mdogo wa Chama cha Ushirika cha Stamico, Hoja Shikome, alisema watajitahidi kutunza mazingira, ili kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan, kwa sera rafiki za sekta ya madini alizoziweka katika serikali yake.