Wachinjiwa nyumbu, pundamilia sensa Karatu

Mkuu wa Mkoa Arusha, John Mongella (wa pili kushoto), akiwa na baadhi ya wawindaji jamii ya Wahadzabe

JAMII ya Wahadzabe wilayani Karatu, mkoani Arusha, wamechinjiwa pundamilia pamoja na nyumbu, ili wawepo kwenye makazi yao wakati makarani wa sensa ya watu na makazi watakapopita kuwahesabu.

Akizungumza mjini Karatu, wakati Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella, alipoenda kukagua maendeleo ya sensa mapema leo, Mratibu wa Sensa Wilaya ya Karatu, Rose Mipango amesema zoezi la sensa limeenda vizuri.

Amesema waliamua kuwachinjia jamii ya Wahadzabe, pundamilia wawili na nyumbu wawili, pamoja na kuwapa ndizi mbivu, ili wawepo katika makazi yao kwa ajili ya kuhesabiwa.

Advertisement

“Wahadzabe chakula chao kikuu ni nyama za kuwinda pamoja na matunda, sisi tumeona tuwapatie chakula, ili tuweze kuwapata na kuwahesabu na zoezi letu limefanikiwa.

“Hili ni kundi maalumu, sababu wao ni wawindaji, hivyo tumeweza kuwahesabu kutokana na kukidhi mahitaji yao kupitia kwa viongozi wao na  tumewahesabu vizuri,” amesema.